#SheriaYaLeo (316/366); Panda mlima.
Kwa sisi binadamu, kukaa kwenye wakati uliopo ni kama kuishi sehemu ya chini ya mlima.
Kile kinachoonekana kwa macho ndiyo kinaathiri maamuzi yetu.
Kupita kwa muda ni sawa na kupanda mlima. Muda unapopita, tunakuwa hatuna tena hisia ambazo zilituathiri kwenye wakati husika.
Tunaweza kujitenga na tukio husika na kuviona vitu kwa uwazi zaisi.
Kadiri tunavyopanda zaidi kwa muda kwenda, ndivyo tunavyoongeza taarifa zaidi kwenye tukio husika. Unachokuwa umejua mwaka mmoja baadaye ni tofauti na ulichokuwa unajua kwenye miezi mitatu.
Ni mazoea yetu binadamu kuathiriwa na vile tunavyoona na kusikia kwenye wakati uliopo. Habari mpya, maoni ya wengine na chochote kinachoonekana kuvuma kwa wakati husika.
Hili ndiyo linafanya watu kuhadaika na vitu vya uongo na vinavyoahidi matokeo ya haraka bila kazi.
Ndiyo pia linafanya upate taharuki pale mambo yanapobadilika.
Kuondokana na hali hiyo, macho yako yanapaswa kuwa kwenye malengo makubwa, ambayo hayaonekani kwa haraka.
Unapaswa kuangalia vitu kwa muda mrefu na kujipa muda kwenye kitu chochote kile.
Kwa mtazamo wa muda mrefu, utakuwa na utulivu na ubayana wa kuweza kufikia lengo lolote.
Usiyumbishwe na mambo unayoyaona kwenye wakati uliopo, kuwa mtulivu na jipe muda, kuna mengi utayajua na kukusaidia kupata unachotaka.
Sheria ya leo; Tengeneza madhara ya muda kwa kujipa mtazamo wa muda mrefu kwenye mambo mbalimbali. Kadiri unavyoona mbali ndivyo unavyoweza kuwa na muda na utulivu wa kufanya maamuzi bora zaidi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji