2816; Kuhimili mikiki mikiki.
Huwa kuna kichekesho ambapo mtu anasema kila akipata ufunguo wa mafanikio, anakuta kitasa kimebadilishwa.
Hivyo inabidi aanze kutafuta tena ufunguo mwingine.
Na akiupata tu, vitasa vinabadilishwa tena.
Sijui kama umeipata picha hapo, maana huo ndiyo uhalisia kamili wa maisha yetu.
Tunaweza kupambana sana ili kupata kitu fulani, tukiamini kwa kupata kitu hicho ndiyo tutayafurahia maisha.
Lakini tunapokipata, ndiyo tunaona tunapaswa kupata kikubwa zaidi ya hapo.
Unaweza kuwa na lengo kubwa, unalojisukuma kulifikia ukiamini kukifikia kutayafanya maisha yako kuwa kamilifu na kuyafurahia.
Lakini unapofikia lengo hilo, unaona malengo mengine makubwa zaidi unayopaswa kuyafikia.
Hivyo maisha yako yote yanakuwa ya kukimbizana na malengo.
Kadhalika kwenye changamoto, unaweza kuwa na changamoto zinazokukabili na kupambana kuzitatua, ukiamini ukishazitatua utakuwa na utulivu mkubwa.
Ni pale unapozitatua changamoto hizo ndiyo zinakuja changamoto nyingine kubwa zaidi ya hizo.
Hivyo kila wakati wa maisha yako unajikuta kuna changamoto unatatua.
Ili kuepuka kukata tamaa, jua hivyo ndivyo maisha yalivyo.
Usijipe matumaini hewa kwamba baada ya kulikabili lililo mbele yako sasa utakuwa na utulivu wa kudumu.
Tambua ukimaliza hilo kuna jingine kubwa zaidi linalofunguka.
Maisha yote ni mikiki mikiki mpaka siku unaondoka hapa duniani.
Mara zote kuwa tayari kukubali na kuhimili mikiki mikiki hiyo.
Usisubirishe wala kuahirisha chochote.
Maisha ndiyo yataenda hivyo siku zote, yaishi kwa ukamilifu wake.
Hatua ya kuchukua;
Kila kinachoendelea kwenye maisha yako ndiyo maisha yenyewe na hakuna wakati kila kitu kitatulia na kuwa sawa kama unavyotaka.
Yaishi maisha yako kwa ukamilifu wake, kwa kukabiliana na kila jambo kwa wakati wake na kuyafurahia maisha kwenye kila hatua.
Tafakari;
Siku utakayoona umeyawezea na kuyapatia maisha, ndiyo siku utakayokuwa umeanza kupata anguko la maisha.
Maisha kutokueleweka na kukosa uhakika ndiyo sehemu ya maisha yenyewe.
Wajibu wako ni kukabiliana na kila linalokuja mbele yako kwa wakati linakuja.
Usiahirishe chochote kwa matumaini ya baadaye.
Maisha ni kile kinachotokea wakati unahangaika na mambo mengine.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed