2830; Matokeo hayadanganyi.
Nimewahi kushirikisha huu mfano, ila nitaurudia tena kwa msisitizo zaidi.
Wakati tupo sekondari, mwalimu wetu wa hesabu alikuwa anasahihisha mitihani kwenye majibu tu.
Hakuwa anajisumbua kuangalia njia.
Wanafunzi tukajadiliana na kuona hilo halipo sawa, hivyo tukamwuliza mwalimu kwa nini hasahihishi njia? Maana anatunyima maksi kwenye njia.
Mwalimu alijibu kwa urahisi; njia ya kweli inaleta majibu ya kweli, kama umekosa jibu la mwisho, sina haja ya kujisumbua na njia.
Kwa kipindi kile bado hatukumwelewa, lakini kadiri ninavyokwenda na maisha, ndiyo naona uhalisia wa kauli hiyo ya mwalimu.
Ni ukweli usiopingika kwamba matokeo ya mwisho hayaji kama ajali. Yanasababishwa na njia ambayo mtu anakuwa amepitia.
Kuna watu unaweza kuwaona wanalalamika kweli. Wanakuambia jinsi wanavyofanya kila kitu kwa usahihi, lakini bado hawapati matokeo mazuri.
Unaweza mpaka kushawishika na kukubaliana nao, kuona labda kuna namna wanakwamishwa.
Lakini nikuhakikishie kitu kimoja rafiki yangu, matokeo yoyote unayoyaona kwa mtu, yamesababishwa.
Kuna namna, mtu mwenyewe amesababisha matokeo ambayo anayapata.
Anaweza kukubishia kabisa kwamba hakuna cha tofauti anachofanya, lakini nikuhakikishie kipo, ni vile tu hakionekani.
Hivyo njia bora ya kujipima wewe mwenyewe na hata kuwapima wengine, siyo kwa kusikiliza maneno ambayo mtu anasema, bali kwa kuangalia matokeo ambayo anayapata.
Matokeo yanadhihirisha wazi yale ambayo mtu anafanya au hafanyi.
Na pale unapoona maneno ya mtu na matokeo haviendani, amini matokeo, huo ndiyo uhalisia wake.
Hatua ya kuchukua;
Pima matokeo yote ambayo umekuwa unayapata kisha linganisha na matarajio uliyokuwa nayo na juhudi ulizoweka. Kama haviendani, mchawi wako unamjua, ni wewe mwenyewe. Angalia ni wapi ambapo unajikwamisha wewe mwenyewe.
Tafakari;
Matokeo hayadanganyi, unaweza kuongea sana na kuahidi mengi, lakini matokeo yatajidhihirisha yenyewe. Kama matokeo unayopata hayaendani na matarajio, kuna mabadiliko unapaswa kuyafanya. Kubali na uyafanye, la sivyo utahangaika sana.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed