2831; Foleni ya kushangaa.
Siku iliyopita nikiwa barabarani nilikutana na foleni ndefu, ambayo ilituchukua muda.
Kwa kuwa halikuwa eneo lililozoeleka kuwa na foleni, nilijiambia patakuwa na ajali mbele ambayo imeziba barabara.
Foleni ikasogea, tulipofika sehemu inayosababisha foleni sikuamini macho yangu.
Barabara ilikuwa nyeupe kabisa, ila kuna gari ilikuwa imeacha barabara na kupinduka. Barabara haikuwa imezibwa kabisa.
Kilichosababisha foleni? Watu kushangaa gari iliyoacha barabara.
Yaani tulipoteza muda kwenye foleni kwa sababu tu watu walikuwa wanashangaa ajali.
Hili lilinifanya nifikiri ni muda kiasi gani tunapoteza kwenye maisha kwa kushangaa mambo yasiyokuwa na tija kwetu.
Pia ni muda kiasi gani tunapotezewa na wengine kwa sababu wanakuwa wanashangaa yasiyokuwa muhimu.
Hatua ya kuchukua;
Jiangalie maeneo yote unayopoteza muda au kupotezewa muda na wengine na jiulize ni mambo gani unayoshangaa au wanayoshangaa yasiyokuwa na tija.
Peleka umakini wako wote kwenye yale mambo yenye tija na mengine yote achana nayo.
Muda wako, nguvu na umakini vipeleke kwenye mambo yenye tija kwako tu, usishangae yasiyo na manufaa kwako.
Tafakari;
Ukikusanya muda wote ambao umekuwa unapoteza kushangaa mambo yasiyokuwa na manufaa kwako, ungeweza kufanya yote ambayo umekuwa unasema huna muda wa kufanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed