2836; Udhaifu ndiyo uimara.
Kwa maisha yetu yote tumekuwa tukidanganywa.
Tumekuwa tunaambiwa tuyafanyie kazi madhaifu yetu kwa kuyaondoa ili tuwe imara.
Hilo linafanyika kwa nia nzuri, ila matokeo yake huwa siyo mazuri.
Pale mtu anapohangaika kuondoa madhaifu yake na kuyageuza kuwa uimara, kinachotokea ni madhaifu hayo yanakuwa makubwa na yenye madhara zaidi, huku uimara wake ukipungua.
Kadiri mtu anatumia muda mwingi kwenye madhaifu, ndiyo anazidi kuyapa nguvu na yanaendelea kumkwamisha.
Badala ya kuhangaika kuyaondoa madhaifu ambayo unayo, unapaswa kuyatumia kwa manufaa.
Hiyo ni kwa sababu kila udhaifu ulionao ni uimara kwako pia.
Udhaifu unakuwa uimara pale unapoyakubali na kutokuhangaika nayo.
Badala yake unapeleka nguvu zako zote kwenye uimara wako, kitu ambacho kinakupa manufaa makubwa.
Pia unapoyakubali madhaifu yako, unajipanga yasikukwamishe, mfano kwa kutafuta mtu mwenye uimara kwenye maeneo ambayo una udhaifu nayo na kushirikiana naye.
Kadhalika, kwa huo huo udhaifu, kuna namna unakuwa na manufaa makubwa kwako. Kwa kushindwa kufanya kitu fulani au kukosa kitu fulani, inakuweka kwenye nafasi nzuri ya kutumia vingine ambavyo vinakufaa zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Orodhesha uimara na madhaifu yote ambayo unayo. Orodhesha yote bila ya kuacha hata moja.
Kwa kila udhaifu ulionao, ukubali kama ulivyo. Usijaribu kuficha, kubadili au kuondoa. Badala yake peleka umakini wako kwenye uimara wako na kutumia udhaifu wowote ulionao kwa manufaa.
Kwa kila udhaifu ulionao, jiulize unawezaje kuwa na manufaa kwako, kisha utumie kwa namna hiyo.
Tafakari;
Chochote unachokipa umakini wako, unakipa nguvu kubwa zaidi. Ukipeleka umakini wako kwenye madhaifu yako, unayapa nguvu zaidi na yanakukwamisha. Lakini ukiyakubali na kupeleka umakini kwenye uimara wako, unaupa nguvu uimara huo na kuweza kufunika udhaifu wowote ulionao.
Hivyo njia pekee ya kushinda udhaifu wako siyo kuufanyia kazi, bali kuukubali kisha kupeleka nguvu zako zote kwenye uimara wako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed