2837; Siyo kwa ajili yako, bali wao.
Kitu kikubwa ninachoendelea kujifunza kwa kina kabisa kwenye safari ya mafanikio ni kwamba ili ufanikiwe, unapaswa kwenda kinyume kabisa na tabia zetu za asili kama binadamu.
Tabia kama uvivu, wivu, chuki, ubinafsi na nyingine, ni sehemu ya asili yetu binadamu. Lakini ukiziendekeza hizo, yaani kujiendea tu vile unavyotaka au wengine wanavyoenda, kushindwa kwenye maisha ni uhakika.
Moja ya tabia ya asili ya kuivuka tunayokwenda kujadiliana leo ni ubinafsi.
Kwa asili, sisi binadamu huwa tunafanya mambo kwa ajili yetu wenyewe.
Tunafanya kitu pale kinapokuwa na maslahi kwetu kwanza.
Kama hakina maslahi kwetu au hatuyaoni maslahi kwa haraka, hatufanyi.
Lakini hilo ni kinyume na safari ya mafanikio, unapofanya jambo lolote kwa ajili yako, huwezi kumshawishi yeyote akubaliane na wewe.
Ili kuwashawishi watu, unapaswa kufanya mambo kwa ajili yao na siyo kwa ajili yako.
Kama ni kitu unauza, ukitaka kumuuzia mtu kwa sababu zako, hakuna namna atakinunua. Utahangaika sana, lakini hakuna atakayeshawishika kununua.
Lakini ukiwauzia watu kwa sababu zao wenyewe, wanashawishika kununua zaidi. Unakuwa umewaonyesha kwa nini wanapaswa kupata hicho unachouza na hilo linakuwa na msukumo mkubwa kwao.
Mara zote jikumbushe hili unapofanya kitu, ipi nia kuu, wewe au wengine.
Kwenye kila mazungumzo unayofanya, kagua maneno unayoyatumia sana. Unatumia MIMI/SISI zaidi au WEWE/NYIE?
Matumizi ya maneno hayo tu ni kiashiria tosha unafanya kwa ajili yako au wengine.
Sisi binadamu wote ni wabinafsi, tunapendelea mambo yenye maslahi kwetu. Lakini sisi tunapaswa kwenda kinyume na asili yetu hiyo, kwa kuweka mbele maslahi ya wengine kabla ya yetu.
Hiyo ndiyo njia yenye ushawishi mkubwa kwa yeyote tunayemlenga.
Hakuna utakayemwonyesha kwamba unajali maslahi yake halafu asishawishike na wewe.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jitafakari unafanya kwa ajili ya nani. Kama ni kwa ajili yako kwanza, jua unapoteza muda wako, hakuna namna utaweza kufanikiwa.
Kwa kila mazungumzo unayofanya na wengine, hesabu mara ngapi umetumia MIMI/SISI na WEWE/NYIE. Ongeza zaidi kutumia WEWE/NYIE ili kujenga ushawishi sahihi kwa watu.
Tafakari;
Kikwazo cha kwanza kuvuka ili kufanikiwa ni mazoea yaliyojengeka ndani yako ambayo yanatokana na asili yako. Hilo ni zoezi gumu kufanya ambalo linahitaji kazi na linaumiza, lakini ni lazima kulifanya kama unataka kupata mafanikio makubwa.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed