2842; Usitapeliwe tena.
Utapeli hautakuja kuisha duniani kwa sababu tatu;
Moja, watu siyo waaminifu. Huwa wapo tayari kutumia njia yoyote hata isiyokuwa halali ili tu kupata wanachotaka.
Mbili, watu hawapendi kufanya kazi. Hivyo hutafuta njia ya mkato ya kupata wanachotaka bila kuweka kazi.
Tatu, watu wanapenda kufuata mkumbo. Wakiona wengi wanakubaliana na kitu, wanaona ni sahihi.
Ili usitapeliwe kamwe kwenye maisha yako, zingatia hayo matatu,
Moja, kuwa mwaminifu. Tumia njia sahihi na halali kutafuta kile unachotaka kupata.
Mbili, penda sana kazi. Kama kitu hakihusishi kazi, kaa nacho mbali.
Tatu, usifuate mkumbo. Fikiria kwa akili yako mwenyewe na kufanya maamuzi bila ya kufuata mkumbo.
Na kiboko ya yote ni kuangalia aina ya watu wanaokimbilia kitu.
Ukitaka kujua kitu ni utapeli, angalia aina ya watu wanaokikubali na kukikimbilia.
Kama kitu kinakimbiliwa na wengi ambao hawapendi kazi na wala hawana misingi wanayoisimamia, kaa nacho mbali.
Pia ukiona watu wanatumia nguvu kubwa sana kutetea uhalali wa kitu, jua hapo kuna shida. Vitu sahihi huwa havihitaji nguvu kubwa kutetewa, huwa vinajidhihirisha wazi.
Ukizingatia haya, kamwe hutakuja kutapeliwa.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila fursa ambayo watu wanaileta kwako, swali la kwanza kuuliza linapaswa kuwa ni kazi gani inayopaswa kufanyika ili kuzalisha faida kubwa unayoambiwa utapata.
Kama swali hilo haliwezi kujibiwa mara moja na kwa majibu yaliyonyooma, kimbia, maana wewe ndiye unayetaka kugeuzwa fursa.
Tafakari;
Kwa jinsi watu wanavyopenda fedha na walivyo wabinafsi, ni nadra sana wakung’ang’anizie fursa yenye manufaa kwako. Ukiona umang’ang’aniziwa fursa fulani, jua wewe ndiyo fursa yenyewe.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed