#SheriaYaLeo (346/366); Mtazamo Wa Utoto.

Kama tutakuwa wa kweli kuhusu maisha yetu, wengi wetu tutakubali kwamba hakuna jipya kwenye maisha yetu.
Kila kitu kinaonekana cha kawaida na hakuna kinachotushangaza.

Kuna kitu kikubwa tunajua kinakosekana kwenye maisha yetu, lakini ni vigumu kujua ni kipi hasa.
Kujaribu kuondokana na hali hiyo, huwa tunahangaika na mambo mbalimbali kama kusafiri, kubadili kazi au biashara na hata kuwa na mahusiano.
Mabadiliko hayo huleta upya wa mwanzoni, lakini upya huo huisha ndani ya muda mfupi na mazoea kurudi.

Njia pekee ya kulikabili hili ni kuiangalia dunia kwa mtazamo wa utoto.
Tulipokuwa watoto, kila kitu kilichotuzunguka kilikuwa kikubwa kuliko sisi.
Hivyo mara zote tulikuwa kwenye hali ya kushangazwa na mambo na vitu mbalimbali vilivyotuzunguka.

Huo ni mtazamo ambao nado tunaweza kuutumia, kwa kuangalia ukubwa wa dunia inayotuzunguka na kushangazwa na mengi yaliyopo.
Hali hiyo itaweza kututoa kwenye mazoea tuliyonayo na yanayotuzuia kufurahia kila tunachofanya au kuwa nacho.

Sheria ya leo; Iangalie dunia kwa mtazamo wa utoto na hutachoshwa nayo au kujenga mazoea.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji