2844; Shtuka ni mtego.
Huwa kuna kichekesho kinasema ukiona choo kwenye ndoto usikitumie, ni mtego huo.
Huenda unakumbuka hili vizuri utotoni, unaota unacheza, unaufurahia mchezo, halafu mkojo unakubana, unaenda kukojoa, unashtuka umekojoa kitandani.
Kwenye maisha kuna mitego mingi inayowanasa watu kwa kukosa umakini wa kujua ni mitego.
Moja wapo ni urahisi wa vitu.
Huwa tunapenda vitu viwe rahisi, lakini kwa asili vitu vizuri havijawahi kuwa rahisi.
Hivyo basi, unapoona kitu ni rahisi, hakina changamoto yoyote, halafu ni kizuri, unapaswa kushtuka, huo ni mtego.
Unapoona mambo yanakwenda tu, kimserereko, bila ya ugumu wowote, halafu ni mambo yenye manufaa makubwa, jua wazi kuna kitu hakipo sawa.
Unaweza usione sasa, lakini jua yatakayotokea baadaye siyo mazuri kama unavyotegemea.
Sisemi kwamba tusipende mambo yanapokuwa rahisi, lakini tunaijua wazi asili ya dunia, chochote kizuri na chenye thamani hakijawahi kuwa rahisi.
Kwa kuujua msingi huu na kuuzingatia mara zote, utajiepusha na mengi ambayo siyo sahihi kwako.
Hatua ya kuchukua;
Kila mambo yanapokuwa rahisi kuliko ulivyotegemea, kaa chini na uchunguze kile unachofanya, kuna mtego utakuwa unakwenda kunasa, ni vyema kushtuka haraka kabla ya kunasa.
Tafakari;
Vitu vyenye thamani havijawahi kuwa rahisi na vitu rahisi huwa havina thamani. Hivyo unapokutana na kitu chenye thamani na kikawa rahisi, usidhani wewe ni mjanja sana, kuna wajanja zaidi yako wameweka mitego, shtuka haraka kabla hujamasa kwenye mitego hiyo.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed