2845; Ni kufanya.
Matokeo ni zao la kufanya.
Haijalishi una mawazo na nia nzuri kiasi gani, kama hutafanya, hakuna matokeo utakayoyapata.
Kuwa chanya au hasi haina maana kama hutafanya.
Kipaumbele chako cha kwanza kinapaswa kuwa ni kufanya.
Kufanya na kelele huwa haviendi pamoja.
Wasiofanya watakuwa na maoni mengi kwako, jinsi gani ambavyo haiwezekani.
Lakini wewe unapaswa kupuuza hayo yote na kufanya.
Kufanya kuna nguvu ya kuleta matokeo ya tofauti, hata kama siyo uliyokuwa unayatarajia.
Kufanya hata kama ni kwa kukosea, kunakupa fursa ya kujifunza kuliko kutokufanya kabisa.
Maisha yako yatahukumiwa na yale uliyofanya, siyo kusema wala nia, bali kufanya.
Dunia imekuwa na wasemaji wengi, waliokuwa na nia nzuri, lakini leo hii tunawaowakumbuka ni wafanyaji.
Dunia imekuwa na wakosoaji wengi, walioona wafanyaji wanakosea, lakini mabadiliko ya kweli yamekuwa yanaletwa na wafanyaji.
Kuna vitu viwili vikubwa unavyohitaji kwenye haya maisha.
Cha kwanza ni kujua kwa hakika nini unachotaka kwenye maisha yako. Hiki ni kile unachokitaka kwa uhakika na haupo tayari kukikosa.
Cha pili ni kufanya ili kupata unachotaka. Na hapo huachi kufanya mpaka umepata unachotaka. Haijalishi unakutana na magumu kiasi gani, haijalishi umeshindwa mara ngapi, wewe unaendelea kufanya, kwa ubora zaidi mpaka upate kile unachotaka.
Ukishajua unachotaka na kuamua kukifanyia kazi, hakuna tena kurudi nyuma. Ni mbele kwa mbele, bila ya kujali umekutana na nini.
Yote yanawezekana, kwa kujua unachotaka na kuamua kufanya kwa nidhamu, kujitoa na msimamo mpaka upate unachotaka.
Hatua ya kuchukua;
Jikumbushe kile hasa unachotaka kwenye maisha, lengo lako kubwa kabisa kwenye maisha yako. Kisha jikumbushe yale unayopaswa kufanya ili kupata hicho unachotaka sana. Kila unapokutana na ugumu na kutaka kukata tamaa, jikumbushe kubwa unalotaka kupata na umuhimu wa kuendelea kufanya. Kama bado hujapata unachotaka, unapaswa kuwa kwenye ufanyaji na siyo kingine chochote.
Tafakari;
Ni bora ufanye kwa kukosea kuliko kutokufanya kabisa. Kwa sababu kupitia kukosea utajifunza jinsi ya kufanya kwa ubora zaidi kitu ambacho huwezi kujifunza bila kufanya. Waache wengine wapoteze muda na nguvu kwenye kusema, kupanga na kukosoa. Wewe egemea kwenye kufanya, kuyatathmini matokeo unayoyapata na kuboresha zaidi ufanyaji wako. Kila mara kaa kwenye kufanya, kuna matokeo mazuri kuliko kutokufanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed