2850; Ushindi kila siku.
Sisi binadamu huwa tunapenda sana ushindi.
Ndiyo maana huwa tupo tayari kushindana hata kwenye mambo yasiyokuwa na tija.
Ile hali ya kushinda tu inatufanya tujisikie vizuri.
Lakini sasa, maisha huwa hayatupi ushindi kirahisi. Huwa yanatupa kila aina ya vikwazo na changamoto ili tu tusipate ushindi.
Na hata pale tunapopata ushindi, ile hali ya kujisikia vizuri huwa haidumu.
Ni ndani ya muda mfupi tu tunarudi kwenye kiu ya kutaka ushindi tena.
Hali hiyo ndiyo imekuwa inapelekea watu wengi kukata tamaa. Pale wanapotaka ushindi sana ila wanakuwa hawaupati, wanaona haina maana ya kuendelea.
Ipo njia moja ya uhakika ya kukupa ushindi kila siku, ambao utakuweka kwenye matumaini na kuendelea bila kukata tamaa.
Njia hiyo ni kuwa na mchakato wako wa kila siku wenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wako.
Unachofanya hapa ni kupanga mambo ambayo utayafanya kila siku bila kuacha na yapo ndani ya uwezo wako, yaani humtegemei mtu mwingine ili kuyafanya.
Mfano wa mambo unayoweza kuweka kwenye mchakato wako wa kila siku;
1. Kuamka mapema.
2. Kufanya tahajudi au kusali.
3. Kupangilia siku yako.
4. Kujifunza kitu kipya.
5. Kuandika, malengo yako, mambo chanya.
6. Kufanya mazoezi.
7. Kushukuru kwa yanayoendelea kwenye maisha yako.
8. Kuthamini na kusifia wengine kwenye mazuri wanayofanya.
9. Kwenda hatua ya ziada kwenye yale unayofanya.
10. Kuifanyia tathmini siku yako.
Kwa kuhakikisha kila siku unakaa kwenye mchakato wako bila kujali nini kinaendelea, unakuwa na uhakika wa ushindi kila siku.
Hata kama dunia inawaka moto, wewe unakaa kwenye mchakato wako bila kuyumba.
Ni ushindi huo wa kila siku ndiyo unakupa mafanikio makubwa kwenye maisha yako, hata kama unapitia magumu kiasi gani.
Tatizo la wengi ni pale wanapopitia changamoto mbalimbali, wanaacha kukaa kwenye mchakato, na hapo ndiyo wanaiona dunia ikiwa imewaelemea.
Hatua ya kuchukua;
Andika mchakato ambao utaufuata kila siku bila kuacha, hata iweje.
Orodhesha mambo yako kumi na uyafanye kweli kila siku hata kama dunia inawaka moto.
Tafakari;
Njia ya uhakika ya kupata ushindi kila siku ni kukaa kwenye mchakato.
Haijalishi nini kinatokea kwenye maisha yako na dunia kwa ujumla, wewe kaa kwenye mchakato.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed