#SheriaYaLeo (358/366); Epuka ukuaji wa kiroho feki.

Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kwenye zama hizi ni wengi kushindwa kujua njia sahihi za ukuaji wa kiroho.
Lengo la dini lilipaswa kuwa njia ya watu kupata ukuaji wa kiroho.
Lakini kwa zama hizi, dini zimeshindwa kuwasaidia watu kwenye hilo.
Badala yake zimewajaza hofu na kuwafanya kuwa watumwa.

Matokeo yake ni watu kutafuta ukuaji wa kiroho feki, ambao hauwafikishi kwenye ukuaji wa kiroho, badala yake unawapa faraja ya muda mfupi na kuwaacha pale pale.

Ukuaji wa kiroho feki ni ule unaotokana na vitu vya nje, ila havileti mabadiliko ya kudumu ndani ya mtu.
Matumizi ya vilevi, ushabiki wa mpira, ufanyaji wa mapenzi na vingine vya aina hiyo, huwa vinaleta msisimko kwa mtu, lakini havileti mabadiliko ya kudumu.
Badala yake vinajenga utegemezi na hatimaye mtu kuwa mteja, kwa kuvitegemea vitu hivyo kila wakati.

Teknolojia mpya tulizonazo sasa pia zimekuwa sehemu ya ukuaji feki wa kiroho. Mfano mitandao ya kijamii, imewafanya watu kuwa tegemezi katika kuitumia, huku ikiwa haina mabadiliko bora inasababisha kwao.

Hata miujiza ya dizi za zama hizi, ni ukuaji wa kiroho feki. Kupewa maji, mafuta au kitambaa ambacho ndiyo chenye muujiza ni kuwapa watu faraja bila ya mabadiliko ya kuleta mabadiliko ya kweli ndani yao.

Ukuaji halisi wa kiroho ni pale mtu anapokutana na kitu au hali na kupelekea kuleta mabadiliko ya kudumu ndani yake.
Inabadili mtazamo wake, inaleta ufunuo kwake na kuiona dunia kwa namna nyingine.
Hilo linafanya mtu kuchukua hatua za tofauti na kuyabadili kabisa maisha yake.

Inaweza kuwa kukutana na changamoto au matatizo makubwa, kupona kwenye ajali ambayo mtu angeweza kufa, kupatwa na ugonjwa usiopona, kujifunza vitu vipya au tafakari inayomfungua mtu kwa upya.

Sheria ya leo; ukuaji feki wa kiroho unatokana na mambo ya nje lakini hauachi mabadiliko ya kudumu ndani ya mtu, badala yake inatengeneza utegemezi. Ukuaji halisi wa kiroho unatokan na mambo ya nje yanayoleta mabadiliko ya kudumu ndani ya mtu.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji