2855; Wewe ni miujiza.

Kupatikana kwako ni tukio la miujiza mikubwa.
Kukutana kwa wazazi wako, lilikuwa tukio ambalo hakuna aliyelitegemea.
Wazazi wako kuamua kufanya mapenzi siku ambayo mimba yako ilitungwa pia ni tukio ambalo huenda lisingetokea. Kama mmoja wao angekuwa amesafiri au kuumwa, siku hiyo zoezi hilo lisingefanyika.

Katika mbegu nyingi ambazo zilitolewa siku hiyo, mbegu iliyokusababisha wewe kushinda ni tukio la miujiza mikubwa. Kungekuwa na uwezekano mkubwa wa mbegu nyingine kupata ushindi na hivyo kuzaliwa mtu mwingine tofauti kabisa.

Lakini pia umevuka changamoto na vikwazo vingi tangu kuzaliwa mpaka sasa. Umekwepa hatari mbalimbali na kuweza kuwa hai mpaka sasa. Ni miujiza mikubwa mno.

Lengo la kujikumbusha yote haya ni uache kujichukulia poa na kujidharau. Kwa miujiza yote iliyotokea kwenye maisha yako mpaka hapo ulipofika sasa, unapaswa kujiheshimu na kujikubali sana.

Unapaswa kuiendeleza miujiza hiyo kwenye maisha yako ili uweze kufanya makubwa.
Na uzuri ni kwamba miujiza yako haijaisha, bado ipo mingi sana, ni wewe kuijua na kuitumia.

Hatua ya kuchukua;
Nguvu ya miujiza bado ipo ndani yako, itumie kufanya makubwa ambayo hayajazoeleka na wengine. Tumia upekee wako kufanya mambo ambayo wengine hawawezi kuyafanya na hayo yatakupa mafanikio makubwa.

Tafakari;
Ukiangalia mlolongo wa matukio yote kwenye maisha yako, kitendo cha wewe kuwa hai mpaka sasa ni miujiza mikubwa. Itumie miujiza hiyo kuendelea kufanya makubwa zaidi. Tayari nguvu hiyo ipo ndani yako, kilichobaki ni wewe kuitumia.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed