2856; Ishi kila siku kama ndiyo siku yako ya mwisho.

Huwa tunaona tuna muda mwingi, mpaka pale tunapokuja kugundua muda wetu umeisha.

Ni rahisi kujiambia utafanya kesho, kwa kuwa umezoea kuziona kesho nyingi.
Lakini ipo siku ambayo hutaiona kesho uliyopanga.
Ubaya ni huwezi kuijua siku hiyo ni ipi.
Lakini uhakika ni ipo.

Ili usiendelee kupoteza muda na kujidanganya kwa kesho usizokuwa na uhakika nazo, unapaswa kuiishi kila siku kama vile ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani.

Acha kujiambia utafanya kesho, badala yake fanya yote leo.
Acha kuahirisha mambo ukiona bado una muda, jua huna muda.

Ishi kila siku kwa ukamilifu wake, ukijua huna siku nyingine.
Na pale unapoiona siku nyingine mpya, ipokee kama zawadi na yenyewe pia iishi kama ya mwisho.

Dhana ya kuishi kila siku kama ndiyo ya mwisho kwako haimaanishi utapanye vitu vyako kwa sababu huna tena muda. Bali inamaanisha utumie vyema muda wako na kwa tija ili uweze kupata matokeo bora.

Hatua ya kuchukua leo;
Fikiria kama ungeambiwa leo ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani, ni mambo gani ungeyapa kipaumbele zaidi? Hayo ndiyo muhimu kwako, yafanyie kazi.
Kila siku mpya unayoianza jiambie ndiyo siku ya mwisho kisha weka vipaumbele sahihi kwa siku hiyo.

Tafakari;
Kuna siku itakuwa ya mwisho kwako hapa duniani. Ubaya ni hujui siku hiyo itakuwa ipi. Hivyo ili kuwa upande salama, chukulia kila siku unayoipata kama ndiyo siku ya mwisho kwako hapa duniani. Kamilisha yote yaliyo muhimu badala ya kuyaahirisha. Fanya hivyo na utaweza kutekeleza mengi makubwa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed