#SheriaYaLeo (364/366); Tafakari maajabu ya dunia.
Kila unachokiona kwenye maisha yako hapa duniani ni maajabu.
Ukianza na mwili wako mwenyewe, una maajabu mengi ambayo huwezi kuyaelezea.
Hujui chanzo cha hisia zako, huwezi kuona ubongo wako wala jinsi chakula kinavyomeng’enywa tumboni kwako.
Lakini hayo yote yanaendelea kwenye mwili wako na unayaona matokeo.
Ukienda kwa wengine, kuna mengi sana ambayo huyaelewi kuhusu wao.
Huna mtazamo ambao wengine wanao. Hujui nini wanafikiria kwenye akili zao na kwa nini.
Huelewi kwa nini wanafanya yale wanayoyafanya.
Kila kitu kuhusu watu wengine ni maajabu kwetu.
Halafu kuna maajabu ya ulimwengu kwa ujumla. Namna dunia inazunguka jua, majira mbalimbali, matetemeko na majanga mengine, yote hayo hatuwezi kuyaelezea kwa uhakika.
Kadiri sayansi na teknolojia inavyokua ndivyo tunazidi kupata uelewa wa maajabu mengi ya dunia na kujua mengine ambayo hatukuwa tunayajua hapo awali.
Kwa kutafakari ukuu na maajabu haya ya dunia tunajionea wazi jinsi kulivyo na fursa ya kuweza kufanya makubwa kuliko tulivyozoea kufanya.
Sheria ya leo; Pale unapokuwa kwenye hali ya kukosa uhakika au kutokujisikia vizuri, tafakari maajabu ya dunia kwa kuanza na wewe mwenyewe, wengine na ulimwengu kwa ujumla. Utaona vitu kwa namna ya tofauti na kuondokana na hali unayokuwa nayo.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji