2861; Nguvu kubwa kuliko wewe.

Ipo nguvu kubwa kuliko wewe ambayo inauendesha huu ulimwengu.
Bado hatuielewi vizuri nguvu hii, hivyi tumekuwa tunaipa majina mbalimbali.
Wapo wanaoiita Mungu, wengine wanaiita Asili na mengine.

Lakini wote tunakubaliana kwamba ipo nguvu kubwa inayofanya ulimwengu mzima uende unavyoenda.
Kuchomoza na kuzama kwa jua, kuonekana kwa nyota angani na mengine ni mambo ambayo hakuna mwanadamu anayeyadhibiti moja kwa moja.

Kutambua uwepo wa nguvu hii ni muhimu, kwani unaweza kujisalimisha kwenye nguvu hiyo na ikakupa mwongozo wa namna ya kuyaendea haya maisha.

Kwa sababu changamoto kuu ya maisha ni kwamba tunakuja bila kitabu cha matumizi. Yaani hukuzaliwa na kitabu chenye maelezo kuhusu wewe, una uwezo na vipaji gani na una kusudi na malengo gani.

Kukosekana kwa maelezo hayo kumepelekea wengi kuzurura kwenye hii dunia bila ya kufanya chochote chenye tija.

Lakini ndani ya mtu tayari yote yapo. Tayari kusudi lipo, vipaji na uwezo pia upo.
Tatizo wengi wamekuwa wanashindwa kufikia kilicho ndani yao kwa kushindwa kutumia nguvu kubwa inayoendesha ulimwengu.

Unaweza kuifikia na kuitumia njia hiyo kwa kufanya sala au tahajudi.
Sala ni mazungumzo kati yako na nguvu kubwa inayouendesha ulimwengu.
Hilo ni eneo ambalo unaweza kufungua pia nguvu kubwa iliyo ndani yako.

Tahajudi ni kutuliza akili yako na kuiunganisha na nguvu kubwa inayoongoza ulimwengu. Kwa njia hiyo unaweza kufungua uwezo mkubwa ulio ndani yako na kutumia nguvu kubwa ya ulimwengu kufanya makubwa.

Kusali na kutahajudi ni vitu ambavyo unapaswa kufanya kila siku. Ni njia ya kujisalimisha kwenye nguvu kuu inayoendesha huu ulimwengu na kuifanya ikuongoze kwa kilicho sahihi kwako kufanya ili maisha yako yawe na tija.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku tenga muda wa kusali na kutahajudi. Haya ni mazoezi mawili muhimu kwako kuyafanya ili uweze kutumia nguvu inayoendesha ulimwengu kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Tafakari;
Ndani yako una nguvu na uwezo mkubwa ambao hakuna mtu yeyote anayeweza kukuonyesha. Ila ukijisalimisha kwenye nguvu kuu inayoendesha ulimwengu, utaweza kujua na kufikia nguvu na uwezo wako mkubwa na kutumia kufanya makubwa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed