#SheriaYaLeo (366/366); Uhuru kamili.

Uhuru kamili kwenye maisha ni kuishinda hofu ya kifo.
Kujifunza jinsi ya kufa ni kuondoka kwenye utumwa wa maisha.
Kujua jinsi ya kufa kunatuweka huru na kila aina ya vikwazo na changamoto.

Tangu enzi na enzi, uwepo wa kifo umekuwa unatupa hofu kubwa.
Hofu hiyo ndiyo imekuwa inatumika kujenga tamaduni, imani, dini, taasisi n jumuia mbalimbali.

Tumekuwa watumwa wa hofu hiyo ya kifo kiasi kwamba ikitumiwa kwetu huwa tunakuwa tayari kukubaliana na chochote.
Chukua mfano wa dini, nyingi zimejenga hofu kwenye kifo na kuchomwa moto siku ya mwisho, kitu kinachowafanya wengi kuwa watumwa wa dini hizo.

Njia pekee ya kuondokana na utumwa huu na kuwa na uhuru kamili wa maisha yetu ni kukipokea na kukikubali kifo.
Kuwa tayari kwa kifo wakati wowote kunakupa uhuru mkubwa kwenye maisha yako.
Kama huogopi kifo, hakuna yeyote anayeweza kukutishia na chochote.

Ukishaivuka hofu ya kifo, huwi na haja ya kujizuia kwenye fikra na matendo yako. Unakuwa na uthubutu wa kuwa wewe, kufikiri kwa akili yako na kufanya kile kilicho sahihi badala ya kufuata mkumbo kwa hofu unayokuwa umejengewa.

Unakuwa tayari kuachana na chochote ambacho hakiendani na vile unavyotaka, kwa sababu unajua hilo litatokea wakati wa kifo chako, ambacho ni uhakika.

Unakuwa tayari kujitoa kweli kwenye kila unachofanya, ukijua muda wako siyo mwingi wa kuweza kupoteza kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

Ivuke hofu ya kifo kwa kukikubali na kukipokea ili uweze kuwa na uhuru kamili wa maisha yako.

Sheria ya leo; Ukishaonja uhuru unaotokana na kuivuka hofu ya kifo, unavutiwa kufanya makubwa zaidi kadiri inavyowezekana. Uhuru huo unakuja na fursa nyingi zaidi kwako.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji