2862; Lazima tuambiane ukweli.
Kwako rafiki yangu unayeyataka mafanikio makubwa,
Kuujua ukweli, ambao ni mchungu ni sehemu ya hii safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
Sababu ya kwanza kwa wengi kushindwa kwenye hii safari ni kutokuukubali ukweli ambao ni mchungu.
Mafanikio makubwa yanawezekana kabisa.
Lakini yanakutaka ujitoe mzima mzima na usijibakize hata kidogo.
Mafanikio makubwa unayoyataka yatakutoa machozi, jasho na damu.
Utahitajika kufanya kazi kuliko wengine wanavyofanya.
Utakutana na magumu na vikwazo vya kila aina ambavyo vitakukwamisha na kukuumiza sana.
Yote hayo hayatokei kwa ajili yako, bali ni njia ya dunia kuhakikisha kwamba mafanikio makubwa yanaenda kwa wale wanaostahili kweli.
Hebu fikiria kama mafanikio makubwa yangekuwa yanapatikana kirahisi na kwa kila mtu!
Yasingekuwa hata na thamani, yangedharaulika na kuchukuliwa kitu cha kawaida.
Mafanikio makubwa yanakutaka ubadili kabisa mfumo wa maisha yako.
Yanakutaka uache kuishi maisha ya kawaida na kuzungukwa na watu wa kawaida.
Wale wanaokuzunguka huwa ndiyo kikwazo kikubwa kwako kupiga hatua kubwa unazopanga kupiga.
Mafanikio makubwa yanakutaka uwe na roho ngumu, ambayo wengine wanaita roho mbaya.
Lazima uwe tayari kuendelea kujisukuma hata pale njia inapokuwa haionekani kabisa.
Umeshajua unachotaka, unapaswa kuendelea kukipambania kwa kila mamna.
Mafanikio makubwa yatakufanya mpweke.
Kuna sababu kwa nini tai huwa wanatuka wenyewe.
Ndege wengi huruka kwa makundi, lakini tai huruka wenyewe.
Kwa sababu kwenye anga za juu kabisa, hakuna wengi.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyojikuta ukiwa mwenyewe.
Mafanikio makubwa yatafanya uchukiwe na watu.
Kitendo tu cha wewe kujituma kuliko wanaokuzunguka, kitawafanya wajisikie vibaya.
Kitawakosesha sababu ya wao kutokufanikiwa na utawafanya waonekane wazembe.
Mafanikio makubwa yana raha yake.
Kwenye kuyapambania utasukumwa kutumia uwezo wote ulio ndani yako.
Na ukishayafikia, utajisikia vizuri kwa muda kisha kuona mafanikio makubwa zaidi unayopaswa kuyapambania.
Huu ndiyo ukweli unaopaswa kuujua kuhusu mafanikio makubwa unayoyataka.
Ni wewe utaamua kama utasuka au utanyoa.
Uache kujidanganya na uamue kweli unayataka mafanikio makubwa na kuyapambania au huyataki na kurudi kwenye maisha ya mazoea.
Hakuna njia ya kati inapokuja kwenye mafanikio.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe