2863; Kama huuzi unafanya nini?
Kwako rafiki yangu mpendwa uliye kwenye biashara.
Unajua kabisa kwamba mauzo ndiyo namba ya kwanza na muhimu kwenye biashara.
Unajua bila mauzo hakuna fedha na bila fedha hakuna biashara.
Haya yote unayajua bila ya shaka yoyote.
Lakini bado huuzi.
Je unategemea nini?
Unajipa sababu mbalimbali.
Lakini sababu hazijawahi kuleta fedha kwenye biashara.
Ni mauzo pekee ndiyo yanayoleta fedha.
Kutokuuza kwenye biashara siyo tu ni uvivu na uzembe, bali pia ni dhambi.
Kwa mfano kama ungekuwa umegundua dawa ya ugonjwa sugu unaowasumbua wengi, halafu ukakaa nayo dawa hiyo wewe mwenyewe, je huoni huo ni ubinafsi na kuwanyima wengine fursa nzuri?
Sasa ndivyo ilivyo kwenye kile ulichonacho ila hukiuzi.
Una bidhaa au huduma ambayo wengine wanaihitaji sana ili maisha yao yaende vizuri.
Lakini huwauzii.
Maana yake wewe ni kikwazo kwao kuendesha maisha yao vizuri.
Kuuza kile ulichonacho ni wajibu wako wa kimaadili kabisa.
Kama huuzi, unawapunja na kuwadhulumu wengine.
Wewe unakuwa chanzo cha wao kuwa na maisha magumu na kukosa yale wanayoyataka sana.
Hivyo basi rafiki yangu, pambana kuuza.
Upo kwenye biashara, wajibu wako wa kwanza ni kuuza.
Hata kama umeajiri wauzaji, wewe ndiye muuzaji wa kwanza, unayepaswa kuwauzia wauzaji wako umuhimu wa wao kuuza zaidi.
Biashara yako kutokuuza hauna wa kumlaumu isipokuwa wewe mwenyewe.
Ni wewe ndiye unaikwamisha biashara yako isifanye mauzo makubwa, kwa sababu hujayapa mauzo kipaumbele cha kwanza.
Kuanzia sasa badilika, kila mara fikiria unaweza ukauzaje zaidi kwenye biashara yako.
Hayo ndiyo mawazo yanayopaswa kutawala fikra zako kwa muda mrefu.
Kwa sababu kadiri unavyokuwa na mawazo haya, ndivyo unavyoziona fursa nyingi zaidi za kuyatekeleza.
Fanya kila unachopaswa kufanya ili uweze kuuza zaidi.
Uzuri wa maisha ni kwamba, chochote unachokipa umakini wako ndiyo huwa kinakua sana.
Kwenye biashara yako, peleka umakini wako wote kwenye mauzo na utaweza kuuza sana.
Swali muhimu la kujiuliza kila mara ni kama huuzi unafanya nini?
Usizurure kwenye biashara yako siku nzima, ukihangaika na yasiyokuwa na tija na kusahau moja lililo muhimu zaidi ambalo ni kuuza.
Uza, uza, uza.
Hicho ndiyo kitu cha kufikiria kila muda kwenye biashara yako.
Ukiweka kipaumbele sahihi kwenye mauzo, lazima utayakuza mauzo yako.
Je unakwenda kufanya nini ili kuuza zaidi leo?
Karibu ushirikishe majibu ya swali hilo ambayo utakwenda kuyafanyia kazi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe