2864; Kama kweli unajua.

Kwako rafiki yangu unayedhani tayari unajua kila kitu na huhitaji tena kujifunza.

Ni kweli unaweza kuwa unajua mengi unayosema unayajua.
Lakini je, matokeo unayozalisha yanaendana na hicho unachosema unajua?

Maana kama unasema unajua, lakini matokeo unayozalisha ni tofauti na unachosema unajua, kuna tatizo mahali.
Huenda hujui kama unavyodhani unajua.

Hivyo badala ya kuleta kiburi na kukataa kujifunza, kuwa mnyenyekevu na ujifunze.
Na kwa kila unachojifunza, kifanyie kazi mara moja kabla hakijapoa.
Chukua hatua kwa yale unayojifunza ili uweze kuzalisha matokeo ya tofauti.

Kwa sababu mwisho wa siku, mafanikio yako hayatapimwa kwa yale unayosema, bali yatapimwa kwa yale uliyofanya na matokeo uliyozalisha.

Kama inabidi utumie muda na nguvu kubwa kuelezea unachojua na uliyofanya, kuna tatizo.
Hujui kama unavyodhani na hujafanya makubwa kama unavyofikiria.

Matokeo ndiyo kipimo kikuu cha ujuzi na kuchukua hatua.
Hivyo jiangalie wewe mwenyewe, je matokeo unayozalisha yanaendana na kile unachosema unajua?
Kama haviendani, ni wakati wa kubadilika ili uweze kuzalisha matokeo ya tofauti.

Chochote unachodhani unajua, kuna mengine mengi sana ambayo bado hujayajua, hivyo unapaswa kuendelea kujifunza.
Na hata yale ambayo tayari umeshajifunza, bado unapaswa kuyarudia rudia kujifunza mpaka yawe sehemu ya maisha yako ya kila siku.

Fikiria wimbo unaoupenda sana na ambao umekuwa unaweza kuuimba bila kusoma mahali. Umeweza hivyo kwa sababu ya kurudia rudia kuuimba wimbo huo kwa muda mrefu.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa mengine unayojifunza, ili yawe sehemu yako yarudie rudie kwa muda mrefu bila kuchoka.
Na muhimu, yafanye kwa vitendo, hakuna chenye nguvu kama kuchukua hatua kwenye yale unayojifunza.

Usikazane kuwapigia watu kelele kwamba unajua, acha matokeo yako yadhihirishe kwamba unajua.
Kazi yako kubwa iwe kuzalisha matokeo yanayotokana na yale unayoyajua.

Kama kweli unajua kama unavyosema unajua, huna haja ya kuwapigia watu kelele kwenye hilo, matokeo yanajionyesha.
Na kama hujui kama unavyosema unajua, pia huna haja ya kuwapigia watu kelele, badala yake kazana kujifunza na kufanya.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe