2865; Hupati matokeo.

Kwako rafiki yangu unayesema hupati matokeo licha ya kuweka juhudi kubwa sana.

Unaona kabisa kwamba umeweka juhudi kubwa, lakini inapokuja kwenye matokeo, yanakuwa tofauti kabisa na ulivyotarajia.

Unaweza kudhani labda huna bahati au una bahati mbaya.
Unaweza kudhani labda juhudi unazoweka siyo sahihi.

Hayo yote siyo kweli.
Tatizo la kutokupata matokeo halitokani na juhudi unazoweka.
Bali linaanzia kwenye namna unavyoweka juhudi hizo.

Matokeo mazuri yanapatikana pale juhudi zinapowekwa kwa msimamo na kwa muda mrefu.
Juhudi zinapowekwa kwa kujirudia rudia bila kuacha, lazima zilete matokeo makubwa na mazuri.

Tone moja la maji halina madhara yoyote kwenye mwamba.
Lakini tone hilo linapojirudia rudia kwa muda mrefu bila kuacha, linavunja mwamba mkubwa.

Hivyo kabla hujakimbilia kusema umeweka juhudi lakini hujapata matokeo, jiulize juhudi hizo umeziweka kwa msimamo na kurudia rudia mara ngapi?

Mifano ipo mingi na ya wazi, ya wengi wakioweza kufanya makubwa kwa kutokukata tamaa kwenye juhudi walizoweka.

Unadhani kwako wewe itakuwa tofauti?
Jibu ni hapana, kanuni za asili zinafanya kazi sawa kwa wote.
Lazima uweke juhudi kwa msimamo na kujirudia mara kwa mara bila ya kuacha.

Swali ni urudie mara ngapi kabla hujakubali kwamba kitu hakifai?
Jibu lipo wazi, unafanya mpaka utakapopata matokeo unayoyataka.
Hujapata matokeo, safari bado.

Hivyo basi rafiki yangu, wewe fanya.
Fanya, fanya, fanya.
Endelea kuboresha ufanyaji wako kadiri unavyokwenda.
Hakuna juhudi unazoweka zikapotea.
Bali zote zinajikusanya na kuleta matokeo bora kabisa.

Nguvu unazokuwa unatumia kwenye kujaribu vitu vingi vipya kila wakati, ukiziweka kwenye kitu kimoja kwa msimamo, lazima upate matokeo bora kabisa.

Kanuni rahisi ninayoweza kukupa ni hii yenye vitu vitatu;
1. Jua kwa hakika nini hasa unachotaka kwenye maisha yako.
2. Jua njia ya kufika au kupata unachotaka.
3. Kaa kwenye njia hiyo bila kuyumba.

Kaa humo na hakuna namna utakosa mafanikio.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe