2868; Mwisho wa changamoto.
Kwako rafiki yangu ambaye unatamani siku moja usingewe na changamoto kabisa.
Umechoshwa na hali ya kila wakati kuwa na changamoto ambayo unakabiliana nayo.
Ukitatua changamoto moja, inaibuka nyingine kubwa zaidi ya hiyo ya awali.
Rafiki, unapaswa kujua kwamba mwisho wa changamoto ni kifo.
Kama bado upo hai, lazima kuna changamoto utakuwa unakabiliana nazo.
Na hasa pale unapokua au kubadilika, ndipo unapokaribisha changamoto kubwa zaidi.
Huwa kuna kichekesho ambacho kimebeba sana uhalisia wa maisha.
Kinaenda kama ifuatavyo;
Ukiwa kijana, unakuwa na muda na nguvu, ila unakuwa huna fedha.
Ukiwa mtu wa makamo, unakuwa na fedha na nguvu, lakini huna muda.
Na ukiwa mzee, unakuwa na muda na fedha, lakini huna nguvu.
Hiyo inatuonyesha jinsi ambavyo hakuna mwisho wa changamoto kwenye maisha yetu.
Hata pale tunapopambana sana na kutatua changamoto kubwa zinazotukabili, tunakuwa tumetengeneza changamoto nyingine kubwa zaidi.
Matamanio yako ya kutokuwa na changamoto kabisa hayaendani na uhalisia wa maisha, hivyo achana nayo.
Changamoto siyo kitu unachopaswa kukikimbia, bali unapaswa kukaribisha ili uweze kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako.
Maana yake ni kwamba, pale unapoona huna changamoto, badala ya kufurahia unapaswa kuwa na wasiwasi kwamba kuna kitu hakipo sawa.
Kama hukutani na changamoto maana yake hakuna mapya na makubwa unayofanya. Upo kwenye mazoea na hivyo unajikwamisha kupiga hatua zaidi.
Hivyo basi, kila unapojikuta ukiwa na changamoto kidogo, tengeneza changamoto kubwa zaidi. Tengeneza changamoto ambazo zitakusukuma ufanye zaidi ya ulivyozoea.
Kama biashara yako haikupi changamoto, tengeneza changamoto mpya za kibiashara.
Anza kwa kujiwekea lengo kubwa zaidi la ukuaji, mfano kukuza mauzo mara mbili.
Ajiri watu wapya ambao watakupa changamoto ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri.
Au pia unaweza hata kuchukua mkopo ambao unakusukuma kufanya matejesho.
Kwa kifupi ni kwamba kama biashara haikupi changamoto, fursa ya ukuaji hapo ni ndogo sana.
Hivyo tengeneza changamoto zaidi zitakazokusukuma ukue zaidi.
Kuna fursa kubwa ya ukuaji kwenye changamoto kuliko kutokuwa na changamoto.
Hivyo zifanye changamoto kuwa rafiki yako, ili uweze kukua zaidi ya hapo ulipo sasa.
Usiombe kutokuwa na changamoto, bali omba uwe imara zaidi ili uweze kukabiliana na changamoto yoyote itakayokukabili.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe