2870; Haifanyi kazi.
Kwako rafiki yangu mpendwa, ambaye umekuwa unatafuta njia ya uhakika na inayofanya kazi.
Umekuwa unajaribu njia mbalimbali, lakini zote umekuwa unaishia njiani kwa sababu hazifanyi kazi.
Wakati unaanza kutumia njia mpya, unakuwa na imani na matumaini makubwa kwamba italeta matokeo makubwa na mazuri.
Ni pale unapoendelea kutumia njia hiyo ndiyo unagundua kwamba siyo rahisi na ya uhakika kama ulivyodhani.
Unaweza kuwa unaweka juhudi kubwa, lakini matokeo unayopata yasiendane kabisa na juhudi unazoweka.
Lakini njia hizo hizo unazoona hazifanyi kazi kwako, kuna wengine wanazotumia na wanapata matokeo mazuri.
Njia hizo zinaonekana rahisi kwao na zenye manufaa makubwa.
Kitu kikubwa unachopaswa kukijua rafiki yangu ni kwamba kila njia inafanya kazi, lakini siyo kirahisi.
Kila njia inafanya kazi kama itafanyiwa kazi kwa msimamo bila kuachwa.
Hilo lina maana kwamba unapaswa kubadili kigezo chako cha kusema kitu hakifanyi kazi.
Inabidi uwe umejaribu kitu mara ngapi ndiyo uhitimishe kwamba hakifanyi kazi?
Unahitaji kuwa na namba kubwa kwenye eneo hilo ili uweze kukaa kwenye mchakato wowote ule kwa muda mrefu.
Kitu moja ambacho tuna uhakika nacho ni hiki; kitu chochote ambacho kitafanyiwa kazi kwa msimamo na kwa muda mrefu, lazima kitazalisha matokeo ya tofauti.
Uzuri ni tunazo hadithi nyingi zinazodhihirisha hilo kwa uhalisia kabisa.
Moja inayosimama sana ni ya Thomas Edison ambaye alijaribu zaidi ya mara elfu 10 ndiyo akafanikiwa kupata taa ya umeme.
Kama angekuwa wa kukata tamaa haraka na kuishia njiani, asingekuwa amefanikisha mengi aliyofanikisha.
Na hata pale Edison alipoulizwa nini kilimsukuma kuendelea licha ya kushindwa mara zote hizo.
Edison alijibu kwamba hajashindwa mara elfu 10, bali alikuwa amegundua njia zaidi ya elfu 10 ambazo hazifanyi kazi. Kwa kuondoa njia hizo ambazo hazifanyi kazi, moja kwa moja akabakiwa na njia zinazofanya kazi.
Tunachoona hapo kwa Edison na ambacho kipo kwa wengi waliofanikiwa ni kuwa na mtazamo sahihi unaowapa matokeo mazuri.
Kwa tukio moja, watu wanaweza kulipokea kwa mitazamo tofauti tofauti.
Hivyo basi rafiki yangu, kabla hujahitimisha kwamba njia fulani haifanyi kazi na ukataka kuachana nayo, jiulize umeshaitumia kwa ubora zaidi mara ngapi?
Usichukulie kama njia haifanyi kazi, bali ichukulie kama njia ya kuboresha ili kupata matokeo bora zaidi.
Ukichagua njia zako vizuri na ukazifanyia kazi kwa uhakika na msimamo, lazima matokeo bora yapatikane.
Kuanzia sasa nenda kalizingatie hili rafiki yangu, kama kuna njia zimefanya kazi kwa wengine, hata kwako pia zitafanya kazi.
Kinachohitajika ni msimamo wako katika kufanyia kazi njia hiyo.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe