2873; Matendo yaendane na maneno.
Kwako rafiki yangu unayesema unayataka mafanikio makubwa, lakini matendo yako hayaashirii hivyo.
Kusema ni rahisi sana, kila mtu anaweza kufanya.
Kupanga ni rahisi, wengi wamekuwa na mipango mizuri.
Ila sasa kuchukua hatua ili kuyapata matokeo ndiyo kugumu na wachache wana ndiyo wamekuwa wanaweza.
Moja ya sababu za wengi kushindwa kwenye maisha ni kujidanganya.
Kusema, kupanga na kuahidi vitu ambavyo hawavitekelezi kiuhalisia.
Wengi wamekuwa wanafuata mkumbo wa yale wengine wanasema na kupanga, wanakuwa kenge kwenye msafara wa mamba.
Inapofika kwenye utekelezaji hakuna wanachofanya, au hata wakifanya, hakiendani na yale waliyopanga na kuahidi.
Unataka kuwa bilionea, halafu sasa;
1. Unalala mpaka usingizi uishe.
2. Unashabikia timu mbalimbali na hupitwi na mchezo wowote.
3. Unakutana na marafiki mara kwa mara kwa ajili ya kustarehe na kuburudika.
4. Upo kwenye kamati za kila aina, jumuiya, harusi, mtaani n.k.
5. Akitokea mtu na kutaka muda wako, anaupata kirahisi tu.
Huko ni kujidanganya na kujilisha upepo. Huwezi kuwa bilionea kwa kuwa mtu wa kawaida.
Lazima uwe mtu wa tofauti sana.
Lazima usieleweke kabisa.
Lazima ukatiwe tamaa na wengine.
Lazima ujiamini na kuwa tayari kusimama mwenyewe hata kama watu wote wanakupinga.
Na hayo yote hayapaswi kuwa mateso kwako, hayapaswi kuwa mambo unayolalamikia.
Bali yanapaswa kuwa vitu ambavyo mtu unapenda kweli kutoka ndani ya moyo wako.
Kwa kifupi lazima uwe na roho mbaya, uwe unafurahia kujitesa wewe mwenyewe.
Wengine wawe wanakuonea huruma kwa namna unavyokwenda.
Lakini kwa upande wako uwe umekubali na kufurahia kila unachofanya na matokeo unayofanya.
Hakuna anayekulazimisha uwe na ndoto au malengo kiasi gani, huo ni uamuzi wako kabisa.
Lakini ukishawaahidi watu kitu, basi hebu hakikisha matendo yako yanaendana na maneno uliyoahidi.
La sivyo utakuwa unajidanganya mwenyewe na kupoteza heshima yako kwa wengine.
Unapoahidi makubwa, tekeleza kwa ukubwa pia ambao haujawahi kutokea ili wanaokuzunguka wakujue kabisa wewe ni mtu wa aina gani na washirikianeje na wewe.
Kama ukiamua tu kutekeleza yale yote umekuwa unapanga na kusema, utaweza kupiga hatua kubwa sana.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe