2874; Asilimia 100.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unataka vitu vyenye matokeo ya asilimia 100.

Leo napenda nikupe ukweli kwamba hakuna chochote kwenye maisha yetu ambacho kinatupa matokeo ya asilimia 100.
Kila kitu kina asilimia chini ya 100.
Na ndivyo maisha yetu yamekuwa yanakwenda hivyo mara zote.

Ukweli mchungu ambao nataka nikupe leo ni kwamba unatumia asilimia 100 kama kichaka cha kuficha uvivu na uzembe wako.
Kwa sababu hutaki kufanyia kazi kitu, unajiambia hakifanyi kazi kwa sababu hakikupi asilimia 100.

Kwa mfano umejifunza mbinu ya mauzo ya kuwapigia simu wateja wako kuwashawishi kuja kununua.
Unapiga simu kwa wateja watano, watatu wanakataa kabisa kununua unachowashawishi wanunue na wawili wanakuambia wakiwa tayari watakuambia.
Unahitimisha kwamba zoezi la simu halina matokeo na unaachana nalo.

Tatizo hapo sito kwamba zoezi la simu halifanyi kazi, bali ni wewe hutaki kulifanyia kazi.
Na hutaki kujiambia huo ukweli kwamba hutaki kulifanyia kazi zoezi hilo, hivyo unajificha kwenye kichaka kwamba kila uliyempigia hakukubali.

Hivi unajua wastani wa ufaulu wa simba?
Simba anayeitwa mfalme wa mwitu, mnyama mkali na mwenye kasi, ufaulu wake ni chini ya asilimia 30.
Yaani katika mawindo yake, simba anafaulu kwa asilimia 30 tu.
Kama atakimbiza wanyama 10 kwa siku, anaishia kukamata wanyama watatu.
Sasa hebu fikiria simba ambaye angekuwa anafikiri kama binadamu. Anajiambia kwa kuwa wanyama 7 nimewakosa, hili zoezi la kukimbiza wanyama halifanyi kazi.
Kwa hakika simba huyo ataishia kufa njaa.

Je umeshaelewa kwa nini unakwama kwenye mengi?
Kwa sababu wakati unaendelea kusubiri upate uhakika wa asilimia 100, ndiyo unaendelea kukosa matokeo ambayo ungeweza kuwa unayapata kama ungechukua hatua.

Rafiki yangu, acha kujidanganya na kujificha kwenye kutaka asilimia 100, fanya kila kinachopaswa kufanyika ili kupata matokeo unayotaka kupata.
Ni bora kufanya kwa kukosea kuliko kutokufanya kabisa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe