2875; Kujiamini na kiburi.
Kwako rafiki yangu unayechanganya kujiamini na kiburi.
Haina ubishi kwamba ili ufanikiwe, lazima ujiamini sana wewe mwenyewe.
Lazima ujiamini kwamba unaweza kufanikiwa.
Na lazima uweze kuvuka wasiwasi na kukatishwa tamaa na wengine.
Ni kujiamini ndiyo kunakuvusha kwenye mambo mengi yanayowakwamisha wengine.
Kujiamini ndiyo kutakuwezesha kuvuka vikwazo mbalimbali unavyokutana navyo kwenye safari yako.
Lakini pia kuna kiburi, ambacho ni kujiamini kulikopitiliza na kusikoendana na uhalisia.
Kiburi ni kudhani hakuna namna unaweza kushindwa.
Mafanikio kidogo unayokuwa umeyapata yanakufanya uone umeshamaliza kila kitu.
Kiburi ndiyo chanzo kikubwa cha wengi wanaopata anguko kubwa baada ya kuwa wamepata mfanikio madogo.
Mafanikio hayo madogo yanawafanya watu hao waone hawawezi kukosea wala kushindwa.
Hilo linawapelekea kuchukua hatua ambazo zinakuwa hatari kubwa kwao.
Ni muhimu sana ujiamini, lakini pia unapaswa kuwa na unyenyekevu.
Haijalishi umepiga hatua kubwa kiasi gani, bado haiondoi uhalisia kwamba unaweza kushindwa.
Hivyo unapaswa kuendelea kuchukua tahadhari, ukipima vizuri hatari zilizopo kwenye kila jambo unalotaka kufanya.
Asili haitakuogopa wewe kwa sababu umefanikiwa. Asili itaendelea kufanya mambo yake na ukichagua kuipuuza itakuadhibu bila huruma.
Amini kwamba unaweza kufanya makubwa unayotaka.
Lakini usidhani kwamba huwezi kushindwa.
Na wala usione mafanikio yoyote uliyoyapata ndiyo umemaliza kila kitu.
Endelea kujifunza,
Endelea kuweka juhudi kubwa,
Bado maisha yana mambo mengi ya kukufundisha.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe