2876; Watu sahihi.

Kwako rafiki yangu ambaye una maono makubwa na unapambana kutafikia ila unakwama.

Mara nyingi sana wanaokukwamisha huwa ni watu.
Watu unaowachagua ushirikiane nao katika maono yako makubwa, wana athari kubwa sana kwenye kuyafikia maono hayo.

Kama unashirikiana na watu sahihi, ambao wameyaelewa maono hayo na wanajitoa kweli ili kuyafikia, kuyafikia inakuwa rahisi.

Kama unashirikiana na watu wasio sahihi, ambao hawajayaelewa maono na hawapo tayari kujitoa, huwezi kuyafikia maono hayo.

Kabla hujaendelea kuweka nguvu kwenye kuyafikia maono yako, anza kuwatathmini wale unaoshirikiana nao.

Kwa bahati mbaya sana tumekuwa tunachukua tu watu ni watu, hatuna vigezo vya kuwachuja.

Kuna sababu watu wapo pale walipo na vile walivyo.
Kama mtu hana kazi yoyote ya kufanya, siyo bahati mbaya, kuna sababu kwa nini hana cha kufanya.

Kama wewe utamchukua bila kujua sababu hizo, maana yake umezihamishia sababu hizo kwako.
Kama zitakuwa sababu na sifa mbaya, zitaishia kukuathiri sana wewe.

Kuhakikisha una watu sahihi ni muhimu sana kwenye mafanikio yako kuliko juhudi unazoweza kuwa unaweka.

Ukiweka juhudi ukiwa na watu sahihi, matokeo yanakuwa mazuri na ya uhakika.

Watu wengi ulionao sasa siyo sahihi, hivyo nenda hatua kwa hatua ukiwasaidia wawe bora na kama hilo litashindikana basi utaachana nao na kupata walio bora.

Zoezi la kupata watu sahihi kwako ni endelevu na linalohitaji muda na uvumilivu.

Na kilicho muhimu zaidi ni wewe mwenyewe uwe mtu sahihi.
Maana mara nyingi huwa unawavutia watu wanaoendana na wewe.
Hivyo kama unapata watu wengi wasio sahihi, jua hata wewe mwenyewe siyo sahihi.

Kuwa sahihi na pata watu sahihi, hakuna ndoto yoyote kubwa utakayoshindwa kuifikia.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe