2878; Wakikuelewa umepotea.

Kwako rafiki yangu unayetaka kupata matokeo makubwa na ya tofauti yanayokupeleka kwenye mafanikio makubwa.

Ili upate matokeo ambayo hujawahi kupata, lazima ufanye mambo ambayo hujawahi kufanya.

Ili upate mafanikio makubwa ambayo wengi hawana, lazima ufanye vitu vya tofauti kabisa na vile wanavyofanya wengi hao.

Na hapo ndipo palipo na hatari.
Kwa sababu unapofanya kitu ambacho wengi hawajawaji kufanya, hawatakuacha kirahisi.
Watakupinga, kukukosoa, kukubeza na kukukatisha tamaa.

Kwa kuwa na kitu ambacho hawajawahi kufanya, wala kuona kikifanyika, wanaona hakiwezekani.

Hivyo unaweza kutumia hali hiyo ya watu kama njia ya kupima usahihi na ukubwa wa wazo unalotaka kufanyia kazi.

Pale unapowaeleza watu wazo lako na wakalielewa, wakalikubali na kukusifia, usifurahie, badala yake umia kwa sababu siyo wazo sahihi.
Kama wengi wanaelewa na kukubaliana na wazo lako jipya, maana yake halina ukubwa wa kutosha na hivyo halitaweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka.

Chochote kinachokubalika na kupokelewa na walio wengi ni cha kawaida sana, ambacho hakiwezi kukupa matokeo makubwa unayoyataka.

Hiki ni kipimo kizuri na cha uhakika ambacho kinakupa majibu sahihi kwa haraka.

Wale wote walioleta mapinduzi na mabadiliko makubwa, hawakukubaliwa kwenye mawazo yao.
Wengi walionekana kama wamechanganyikiwa, kwa sababu mawazo waliyokuwa nayo hayakuwa yamezoeleka.
Walikomaa na mawazo hayo na leo hii tunayafurahia matunda yao.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa pia, kuwa na mawazo ya tofauti na kuyafanyia kazi ili kupata matokeo ya tofauti na makubwa.

Pale wengi wanapokuelewa na kukubaliana na wewe, ni wakati wa kujitathmini wapi unapokosea.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe