2879; Mazingira matatu ya watu kuiba.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayesumbuliwa na wafanyakazi wenye tabia ya wizi.

Unaweza kudhani kwamba tatizo ni hujapata wafanyakazi sahihi ambao siyo wezi.
Lakini huo siyo ukweli, tatizo la wizi kwenye biashara yako, na hata kwenye maeneo mengine ya maisha yako linakwenda zaidi ya tabia za watu.

Asili ya binadamu iko hivi;
Kuna asilimia 5 ambao kamwe hawataiba au kudanganya hata mazingira yaweje.
Kuna asilimia 5 ambao lazima wataiba au kudangajya hata mazingira yaweje.
Halafu sasa kuna asilimia 90 ambao kuiba au kudanganya kwao kunategemea na mazingira.

Watu karibu wote wataiba na kudanganya kama kukiwa na mazingira haya matatu;

Moja wana uhitaji mkubwa na wanaona hawana namna nyingine. Hapo wanasukumwa kuiba na kudanganya ili wapate wanachotaka.

Mbili wanaweza kuhalalisha tabia yao hiyo na kuona ni sahihi kwao kufanya hivyo. Mfano mtu anapojiambia kila mtu anaiba au kudanganya.

Tatu hawezi kujulikana kama ameiba au kudanganya.

Huenda kwa kusoma hapa umejiambia utapambana uwapate asilimia 5 ambao kamwe hawaibi wala kudanganya, lakini uwijidanganye kwenye hilo, watu hao ni wachache sana na vigumu kuwapata.

Njia kubwa unayoweza kutumia kudhibiti wizi na udanganyifu kwenye biashara, kazi na hata maeneo mengine ya maisha yako ni kuondoa mazingira namba tatu.
Yaani kuhakikisha kwamba hakuna namna mtu anayeiba au kufanya udanganyifu anaweza kujificha.

Hilo linawezekana kwa kuweka mifumo sahihi ambayo ni vigumu sana kwa mfu yeyote yule kuilaghai na kujinufaisha binafsi.
Unahitaji udhibiti wa hali ya juu sana kwenye kila eneo la biashara, kazi na maisha kwa ujumla ili kuondosha tamaa za watu kuiba.

Tukichukua mfano wa benki, huwa zinaajiri watu ambao hata bado hazinawajua vizuri tabia zao.
Lakini madhara ya watu hao kwenye biashara, hasa kwenye wizi na udanganyifu huwa hayatokei kwa sababu kuna mifumo inayodhibiti kila kitu.
Ni vigumu sana mfanyakazi wa benki kuondoka na hata elfu moja bila mfumo mzima kujua.

Je kwenye biashara yako, upo mfumo wa kudhibiti watu wasiine?
Kwa sababu hata ukisema unabadili wafanyakazi kwa sababu wanakuibia, kama utawaleta wapya kwenye mazingira yasiyo na udhibiti, ni swala la muda tu kabla nao hawajaanza kukuibia.

Weka mifumo sahihi ya udhibiti kwenye biashara yako na mengine unayofanya kwa kushirikiana na watu wengine.

Tusijaribu kwenda kinyume na asili ya binadamu, tutajitesa, kujiumiza na kujichosha.
Tuitumie asili ya binadamu kwa namna bora kwetu kupata kile tunachotaka.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe