2880; Hasi mara Chanya.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayedhani una nguvu ya kuweza kuwashinda wale wanaokuzunguka.
Kama unazikumbuka vizuri hesabu za magazijuto, ukichukua namba yoyote chanya, ukazidisha na namba yoyote hasi, jibu litakuja hasi.
Hata kama ile namba chanya ni kubwa kuliko hasi.
Yaani -5 × 10,000 = -50,000.
Unajifunza nini hapo?
Kikubwa cha kujifunza ni hiki, hasi ina nguvu ya kushusha sana thamani ya kitu.
Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha.
Unapozungukwa na kushirikiana na watu hasi, haitakuchukua muda na wewe utakuwa hasi kama wao.
Unaweza kujiambia hawawezi kukugeuza kuwa hasi, kwamba wewe ni mjanja, unashirikiana nao kwa yale chanya na kutoondoka na hasi waliyonayo.
Lakini ukweli ni unajidanganya.
Huna huo ujanja wala uwezo wa kukaa na watu hasi halafu ukaepuka wasikuambukize uhasi wao.
Kadhalika kwenye tabia, kiu ya mafanikio, kazi, mahusiano na hata mafanikio.
Imeshasemwa na nitarudia tena kusema hapa, hapo ulipo sasa ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, unaotumia nao muda wako mwingi.
Kama unataka kutoka hapo ulipo sasa, hatua ya kwanza ni kuwabadili wale wanaokuzunguka na unaotumia nao muda wako mwingi.
Muda na nguvu zako ni rasilimali zenye uhaba mkubwa, usizitawanye kwa kujaribu vitu ambavyo utaishia kushindwa.
Peleka rasilimali hizo kwenye vitu vinavyozalisha na kukufikisha unachotaka.
Amua sasa kuachana na wote ambao hawapo kwenye mwelekeo wa kufanya makubwa kama unavyotazamia wewe.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe