2881; Kama hujasikia kwa masikio yako ni umbea.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayejipa sababu za kukwepa kuwakabili wateja wako.

Umepanga vizuri kabisa kwamba utawapigia siku na kuwatembelea wateja wako.
Umejiwekea idadi ya wangapi utawapigia simu na wangapi utawatembelea.

Lakini unapofika wakati wa kutekeleza hayo uliyopanga, ndipo sababu na visingizio mbalimbali vinaibuka kukuzuia usitekeleze uliyopanga.

Unajiambia kabisa huyu mteja hatakubali kununua, hivyo unaamua usimpigie simu au kumtembelea.
Hapo unakuwa umeacha kutekeleza yale uliyopanga, siyo kwa sababu wateja wamekuambia, bali kwa sababu umejiambia wewe mwenyewe.

Leo nakwenda kukupa dawa ya kulivuka tatizo hilo la kuwakimbia wateja kwa sababu za kujipa mwenyewe.

Dawa hiyo ni mtazamo kwamba kama kitu hujakisikia kwa masikio yako mwenyewe, basi ni uongo, uzushi na umbea.
Chochote kile unachojiambia mteja atakujibu, kama bado hajakujibu kweli siyo kweli.
Ni wajibu wako kusikia kwa masikio yako kutoka kwenye kinywa cha wateja ndiyo ufanye maamuzi.

Njia hii ina nguvu kubwa sana kwa sababu kama utampa kila mteja nafasi ya kumsikiliza, utajifunza mengi na kuna ambao watashawishika na wewe.
Kujipa mwenyewe majibu bila ya kuwafikia wateja unaowalenga ni kujipa majibu yasiyo sahihi.

Hata kama unajiambia mtu atakujibu vibaya na kukutukana, jiambie unapaswa usikie hayo kutoka kwa mtu mwenyewe. Hivyo unapaswa kukamilisha uliyopanga kufanya bila kujipa sababu za kutokutekeleza.

Wape watu nafasi, watakushangaza kwa namna watakavyokupokea na kukupa ushirikiano mkubwa.
Na mara zote jikumbushe kama hujasikia kutoka kwenye kinywa cha mtu mwenyewe, huo ni uongo, uzushi na umbea, uepuke kwa gharama zote.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe