2882; Hawaoni unachoona.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayeshangazwa na jinsi watu wanavyoshindwa kufanya yale unayotegemea wayafanye.
Unaweza kuwa umewaeleza kabisa nini wanapaswa kufanya na wanapaswa kukifanyaje.
Lakini wanapokwenda kufanya, wanafanya tofauti kabisa na unavyotegemea wafanye.
Unaweza kushangazwa sana na hilo na hata kukosa imani na watu.
Lakini kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba watu hao hawaoni kile unachoona wewe.
Na watu huwa hawafanyi kile wanachoambiwa, bali wanafanya kile wanachoona.
Maelezo yoyote unayowapa watu, huwa wanayatumia kutengeneza picha fulani kwenye fikra zao, kisha wanafanya kulingana na picha hizo.
Wewe unaweza kushangazwa na kile walichofanya, lakini kwao ni sahihi kabisa, kulingana na picha wanayokuwa nayo.
Hivyo basi, kama unataka mtu afanye vile unavyotaka, msaidie kwanza aone picha unayoiona wewe.
Wape maono uliyonayo juu ya kile unachofanya na hakikisha wamejenga picha sahihi kwenye fikra zao.
Wakishaipata picha hiyo kwa usahihi, wataweza kufanya vile unavyowategemea wafanye.
Wengi wanashindwa kuwatengenezea watu picha sahihi kwa sababu ni kitu kinachohitaji kuweka juhudi.
Ni kitu kisichotaka kabisa uvivu.
Sasa kwa kuwa watu wengi huwa hawapendi kujisumbua, huona bora tu watu wafanye wanavyofanya.
Wewe usiwe hivyo,
Ondokana na kila aina ya uvivu na uzembe.
Unapotaka kitu chako kifanyike, hakikisha unayempa akifanye amepata picha kamili uliyonayo kwenye fikra zako.
Kupata matokeo makubwa na mazuri ni jambo linalotaka juhudi kubwa na za ziada.
Juhudi hizo zinawezekana pale watu wanapokuwa wanajiona kwa namna fulani.
Tayari unayo picha kwenye fikra zako, wasaidie wengine nao waione ili waweze kufanya kwa usahihi.
Hakuna mtu anayeweza kuzisoma fikra zako, hivyo lazima uweke juhudi kuiweka picha hiyo kwenye fikra za wengine.
Siyo zoezi rahisi, ila linawezekana na lina matokeo makubwa.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe