2884; Usiuze, Sikiliza.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayeona mauzo ni magumu na wateja hawataki unachouza.

Utakwama kwenye mauzo kama unachofanya ni kuwalazimisha wateja kununua.

Hata kama ni kitu ambacho tayari wanakihitaji, kitendo cha wewe kuwalazimisha wanunue inawafanya wawe na wasiwasi ambao unawafanya wasiwe tayari kununua.

Ukijikuta inabidi uwalazimishe au hata kuwaomba wateja wanunue, jua kuna kosa umefanya mahali.

Na sehemu kubwa ya kosa inakuwa ni kukimbilia kuuza badala ya kusikiliza.

Msingi mkuu wa mauzo ni kusikiliza.

Kwa sababu unachohitaji kwenye mauzo siyo kumlazimisha mjeta anunue, bali kumjua mteja sahihi wa kile unachouza na kujenga uaminifu.

Kama ukimjua mteja sahihi wa kile unachouza na ukajenga kuaminika naye, kamwe hutalazimisha wateja wanunue, badala yake watakuwa wanakulazimisha uwauzie.

Yaani badala ya kuwakimbilia wateja na kuwalazimisha au kuwaomba wanunue, wateja wanakuwa wanakukimbilia wewe wakikuomba uwauzie.

Hebu pata picha mauzo kwako yatakuwa rahisi kiasi gani pale wateja wanapokuja kwako kukuomba uwauzie.

Sasa tukibaki hapo kwenye urahisi, ili matokeo ya mwisho yawe rahisi, kazi ngumu lazima ifanyike mwanzoni.
Kama utataka kufanya kazi rahisi mwanzoni, matokeo ya mwisho lazima yawe magumu.

Yaani, mauzo ni magumu kwa wengi kwa sababu wanatafuta njia rahisi ya kuyafanya.
Wanaona kila mmoja ni mteja na anapaswa kununua.
Ndiyo maana wanalazimisha na hata kuwaomba wateja wanunue.

Ili mauzo yawe rahisi, lazima kazi ngumu ifanyike kabla ya mauzo.
Na kazi hiyo ni kusikiliza ili kuwajua wateja sahihi, kisha kujenga nao mahusiano mazuri ili wakuamini na kuwa tayari kununua kwako.

Najua unachofikiria, kwamba hilo ni zoezi gumu na refu, huna muda wa kulifanya.
Na hapo rafiki yangu ndiyo unakuwa umethibitisha kwa nini mauzo yanakuwa magumu kwako.

Leo nenda kajifanyie mapinduzi ya kifikra, tambua wajibu wako siyo kuuza, bali kuwajua wateja sahihi na kujenga nao mahusiano bora.

Mauzo yanakuwa rahisi pale unapokuwa na mteja sahihi na anayekuamini.
Kwa mteja wa aina hiyo, humlazimishi kununua, bali unampa mapendekezo ambayo atakuwa tayari kuyafuata.

Ni kanuni ya maisha kwamba chochote unachotafuta kukifanya kwa urahisi, matokeo yake huwa magumu. Na kile unachokifanya kwa ugumu, matokeo yake huwa rahisi.

Usikimbilie kulazimisha au kuomba kila mtu anunue unachouza.
Wewe jua wateja sahihi wa kile unachouza kisha jenga nao mahusiano mazuri.
Mauzo yatakuwa rahisi kwa sababu wao ndiyo watakuwa wanakuomba uwauzie.

Uliza maswali,
Sikiliza,
Jali.
Hayo yatakuweka mbele zaidi kuliko mengine unayoweza kuwa unahangaika nayo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe