2885; Viwango.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayeshangazwa na jinsi ambavyo watu wanakuangusha.
Unakubaliana na watu wafanye kitu fulani, ila wanachofanya kinakuwa tofauti kabisa na mlivyokubaliana.
Hali hiyo inaweza kukufanya upoteze imani na watu, uone haina haja ya kuwategemea watu, bora ufanye kila kitu peke yako.
Lakini unajua wazi ya kwamba huwezi kufanya kila kitu peke yako kama unataka mafanikio makubwa.
Unahitaji sana msaada wa wengine.
Kitu kikubwa unachopaswa kujua na kukumbuka mara zote ni kwamba watu hawakupi kile unachotaka, bali wanakupa kile unachovumilia.
Yaani watu watajaribu kukupa kilicho kidogo au dhaifu iwezekanavyo, kama tu utapokea katika viwango hivyo.
Na kama utakataa kukubali na kupokea vitu vya aina hiyo, watu hawatapata ujasiri wa kukupa.
Kwa maana hiyo basi, mahali unapopaswa kuanzia ni kwenye viwango.
Unapaswa kujiwekea viwango ambavyo hutakubali chochote chini ya hapo.
Na viwango hivyo unaanza kuvisimamia wewe mwenyewe kabla ya wengine.
Yaani wewe mwenyewe hukubali kujipa chini ya viwango vyako.
Na hapo sasa, wengine wote watachagua kukupa viwango vyako au kuachana na wewe.
Unaweza kuhofia kwamba kwa kuweka viwango utakosa watu wa kushirikiana nao.
Unaona wengi watavikimbia viwango vyako.
Lakini ukweli ni kinyume kabisa na hilo. Unapoweka viwango na kuvisimamia, unawaondoa watu wasio sahihi na kubaki na wale walio sahihi na bora kabisa.
Ndiyo kuna watu watakukimbia kutokana na viwango vyako, lakini ni watu ambao wasingeweza kukusaidia chochote. Yaani ni watu waliokuwepo kwako kwa maslahi yao binafsi, bila kujali maslahi yako.
Jiwekee viwango vyako na fia kwenye kuvisimamia.
Usikubali kwa namna yoyote ile kupokea chini ya viwango vyako.
Na yeyote yule, kuanzia wewe mwenyewe, anapaswa kuvifikia viwango vyako au kuangalia utaratibu mwingine.
Viwango vitakusaidia kupata matokeo bora na kwa msimamo mara zote.
Kuwa mtu wa viwango mara zote na watu sahihi watakuja na kukaa kwako.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe