2886; Ameona wapi?

Kwako rafiki yangu unayeshangazwa na yale ambayo watu wanayafanya, hasa ambao ulitegemea wafanye namna fulani.

Kama una mtoto mdogo nyumbani, halafu siku moja ukasikia anatukana, unajua wazi kwamba kuna mahali mtoto huyo amesikia tusi hilo na kujifunza.
Unajua kabisa haijatokea tu, kuna mahali ameona au kusikia na kuona ni sawa na yeye kufanya hivyo pia.
Huenda ni nyumbani au nje ya nyumbani.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwachukulia watu wengine wote unaojihusisha nao.
Unapoona watu wanafanya mambo ambayo yanakushangaza, badala ya kushangaa, jiulize wameona wapi mambo ya aina hiyo yakifanywa.

Kama ni watu unaojihusisha nao, huenda wameona kwako au waliona kwa wengine na wakaona itakuwa sawa hata kwako pia.

Kama una wafanyakazi ambao wanachelewa kazini, wewe jiulize waliona wapi?
Je ni wewe umekuwa ukichelewa kazini hivyo wakaona ni sawa hata wao kuchelewa?
Au ni tabia waliyotoka nayo huko walikotoka, ila wakaona hata kwako inakubalika?

Kwa vyovyote vile, kile watu wanafanya kwako, huenda walikiona kwako au wameona kinakubalika kwako.

Watu hawajifanyii tu kitu bila kuona au kudhani kinakubalika.
Hapo ndipo pa kuanzia kama unataka kubadili yale watu wanayokufanyia.
Hakikisha umewaonyesha kilicho sahihi kufanyika na kama wana mengine wamejifunza huko wanakotoka, usiwape nafasi ya kuyafanya kwako.

Wameona wapi ni swali la kwanza kujiuliza na kujijibu kabla hujaanza kuhangaika na yale watu wanafanya au kutokufanya.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe