2887; Wametoa wapi huo ujasiri?

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unashangazwa na yale ambayo watu wanafanya, ambayo ni tofauti kabisa na makubaliano yenu.

Watu huwa hawafanyi kitu kama hawana uhakika.
Hiyo ni tabia yetu binadamu, kutaka uhakika kabla hatujafanya kitu.

Unapoona watu wamefanya kitu fulani, juna kuna uhakika fulani walio nao ambao unawapa ujasiri.

Wakati mwingine unaweza kuwa tu ni ujasiri wa ujinga, yaani kutokujua madhara ya kitu wanachofanya, hivyo wanajiamini na kufanya.

Pale watu wanapofanya mambo ambayo hukutegemea wafanye, au kutokufanya wanayotakiwa wafanye, anza kwa kujiuliza wanapata wapi huo ujasiri.

Kwa kuanzia hapo utaweza kujua sababu halisi na kuweza kuchukua hatua sahihi zitakazoleta mabadiliko.

Kwa mfano kama una wafanyakazi, ambao unawapa maelekezo ya mambo wanayopaswa kuyafanya, lakini hawayafanyi, lazima kuna kitu kinachokuwa kinawapa ujasiri kwamba hata wasipofanya huna cha kuwafanya.
Ni vyema kwanza ujue hicho kinachowapa ujasiri kabla hujaendelea kuhangaika na kuwafanya watekeleze wanayopaswa kutekeleza.

Kuna vitu vingi vinavyoweza kuwapa watu ujasiri wa kufanya vile wanavyoamua wao, hata kama ni kinyume kabisa na utaratibu.

Cha kwanza kinaweza kuwa mazoea. Hakuna kitu kinawapa watu uhakika na ujasiri kama mazoea. Watu huendelea kufanya vile walivyozoea.
Unapotaka kuleta mabadiliko, anza kwa kuvunja mazoea yaliyokuwepo.

Cha pili kinaweza kuwa ujinga. Watu wanapokuwa hawajui huwa wanakuwa na uhakika na kujiamini sana. Wanapokuwa hawana uelewa wa madhara ya kile wanachofanya, huwa na ujasiri wa kufanya hata kama ni hatari. Kuleta mabadiliko, mfanye kila mtu ajue na kuona hatari ya yale anayofanya.

Cha tatu ni mtu kujiona ni wa juu kuliko wengine na anahitajika sana. Mtu anaona kwamba bila uwepo wake mambo hayawezi kwenda. Kwa utegemezi unaokuwa umejengwa kwake, anaona bila yeye hakuna kinachoenda. Hilo linampa ujasiri wa kufanya anavyoamua yeye, hata kama ni nje ya utaratibu.
Kwa kila unayeshirikiana naye, mfanye ajue na aone wazi kwamba hakuna mtu ambaye hawezi kuondolewa. Wajue hata wewe mwenyewe unaweza kuondolewa na bado mambo yakaenda. Hilo litawafanya watu wajue nafasi zao na kukaa hapo kwa kutulia.

Waswahili wana usemi kwamba ukimkuta kobe juu ya mti, jua amepandishwa hapo.
Kadhalika, unapokuwa na watu ambao hawafanyi wanachopaswa kufanyika, kuna kitu kinakuwa kinawapa ujasiri. Anza kwa kujua na kuondoa kitu hicho ili watu waweze kutekeleza yale wanayopaswa kuyatekeleza.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe