2890; Wanadhani wana akili kuliko wewe.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye wafanyakazi wako wanakataa viwango vipya unavyoanzisha.

Una kiu kubwa ya kujenga na kukuza biashara yako. Unataka kujenga mfumo wa biashara, uwe na timu bora na ufanye mauzo makubwa.

Unaingia gharama ya kupata maarifa na mafunzo sahihi ya kukamilisha hilo.
Unakuwa tayari kuwekeza hasa, ukijua itakulipa vizuri baadaye.

Lakini sasa, watu ambao ulitegemea wapokee vizuri juhudi hizo unazoweka, wanakuwa wa kwanza kukupinga.
Wafanyakazi wako, ambao ndiyo timu unayokazana kujenga, wanakataa kuendana na mambo mapya unayoanzisha.

Unawalipia wapate mafunzo, ambayo yatakuwa na manufaa kwao hata baada ya kuondoka kwenye biashara yako. Lakini bado wanakugomea kujifunza mambo hayo mazuri, ambayo unaingia gharama wayapate.

Unaanzisha viwango vipya vya ufanyaji kazi na uendeshaji wa biashara yako, viwango ambavyo kila mtu akivifuata, matokeo mazuri na makubwa yatazalishwa.
Lakini wanakataa viwango hivyo na kuendelea na mazoea yao.

Kama umekuwa unashangazwa na hali hiyo, leo nakwenda kukufumbua macho.
Usidhani kwamba hawajui wanachofanya, wanajua sana na wanafanya kwa makusudi.

Wanachoona wao ni kwamba wana akili kuliko wewe.
Ndiyo, wanaona wazi kwamba hayo mambo yako mapya unayokuja nayo ni ujinga mtupu na hawapo tayari kuendana na ujinga huo.

Wanaona walichozoea kufanya wao ndiyo kilicho sahihi na bora na mapya unayokuja nayo hayana maana.

Hawatakuambia yote hayo, lakini hizo ndizo fikra zao.
Hivyo wakati wewe unawasubiria waelewe mabadiliko unayoleta na wayakubali, wao wanasubiri mabadiliko hayo yashindwe na wakucheke nyuma ya mgongo wako.

Ujumbe wangu wa leo ni wa kukupa nguvu na ujasiri wa kupambania mabadiliko unayoleta kwenye biashara yako.

Na ujasiri mkuu ninaotaka kukupa ni huu; wewe ndiye mwenye akili kuliko wafanyakazi wako, bila ya kujali wamekuzidi elimu kiasi gani.
Kitendo cha kwamba wewe umeweza kuanzisha biashara na kuwaajiri, inamaanisha kuna kitu unacho na wao hawana.
Lazima ukitambue na kukitumia kitu hicho.

Ukipuuza hicho, wafanyakazi wako wataiteka biashara yako na wewe utakuwa kama mateka.
Na kitakachokwenda kutokea ni biashara kupata anguko kubwa.

Sisemi usichukue maoni ya wafanyakazi wako au uwadharau, la hasha.
Chukua maoni yao utakavyo, waheshimu kwa mchango wanaotoa kwenye biashara yako.

Lakini inapokuja kwenye mabadiliko unayotaka kuleta kwenye biashara yako, inapokuja kwenye kuweka viwango vya juu, lazima kila aliye kwenye biashara yako akubaliane nayo.
Usilegeze hata kidogo kwenye maeneo hayo.
Waeleze wazi kwamba mabadiliko na viwango vipya ndiyo utaratibu uliopo na wa kudumu.
Waeleze hakuna namna ya kurudi nyuma.
Kila mmoja akubali kuendana na mwenendo mpya au ajiweke pembeni.

Naeleza hili kwa wazi na ukali kwa sababu naendelea kuona ukinzani ambao wengi mnakutana nao katika kuleta mabadiliko na kuanzisha viwango vipya vya ufanisi.
Usikubali kukwamishwa na yeyote yule.
Una nia njema ya kupiga hatua kubwa, pambania hilo bila kukubali kutetereshwa na lolote.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe