2893; Vinavyofundishika na visivyofundishika.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unajaribu kuwafundisha wafanyakazi wako lakini hawafundishiki.

Kuna vitu huwa vinafundishika kwa watu kirahisi na kuna vitu ambavyo havifundishiki kirahisi.

Jinsi ya kuifanya kazi ni kitu ambacho kila mtu anaweza kufundishwa.
Na kama ataweka umakini kwenye hilo, ataweza kuelewa na kufanya vizuri.

Tabia na mtazamo sahihi wa kuwa nao kwenye kazi ni vitu ambavyo huwezi kuwafundisha watu.
Tabia na mtazamo ni vitu vinavyokuwa ndani ya mtu, ambavyo siyo rahisi kuvibadili.

Unaweza kufundisha tabia na mtazamo utakavyo, lakini kama haijatoka ndani ya watu kweli, hakuna kitakachobadilika.

Kwa uhalisia huu, unapaswa kubadili sana namna unavyoajiri wafanyakazi kwenye biashara yako.
Wakati wa kuajiri, kipaumbele cha kwanza kiwe kwenye yale yasiyofundishika.
Yaani angalia kwanza uwepo wa yale yasiyofundishika kabla ya yale yanayofundishika.

Angalia kwanza uwepo wa tabia na mtazamo unaoutaka kabla ya ujuzi.
Kama mtu ana tabia na mtazamo sahihi, kumfundisha jinsi ya kuifanya kazi ni rahisi. Tena tabia na mtazamo wake vinalirahisisha sana zoezi.
Lakini kama hawana tabia na mtazamo sahihi, hata kama tayari wanao ujuzi unaoutaka, watakusumbua sana.

Matatizo mengi kwenye kuajiri yamekuwa yanatokana na watu kwenda kinyume na hilo.
Kigezo chao cha kwanza kwenye kuajiri kinakuwa ujuzi wa kufanya majukumu ya kazi. Tabia na mtazamo havipewi uzito.

Kinachokuja kuwakwamisha watu kwenye kazi siyo ujuzi, bali tabia na mtazamo. Ndiyo maana hivyo ni muhimu kuanza navyo mapema kabisa.

Tena ni bora kuajiri watu ambao hawana uzoefu kabisa, ili uwafundishe wewe namna sahihi ya kufanya mambo.
Wenye uzoefu wa kazi mara nyingi wanakuwa na mitizamo isiyo sahihi juu ya kazi husika.
Inakuwa kazi ngumu sana kwako kuvunja mitizamo hiyo ambayo imeshaota mizizi kwao.

Ukiajiri wenye uzoefu, tayari wanakuwa wanajua nini kinaweza na nini hakiwezi kufanyika, hivyo wanakuwa wameshajiwekea ukomo.
Ukiajiri wasio na uzoefu, hawajui nini kinawezekana na nini hakiwezekani, hivyo wanakuwa hawana ukomo wowote, watafanya kila unachowafundisha kufanya.

Ajiri watu wenye tabia njema, wenye shauku kubwa na mtazamo chanya wa uwezekano.
Kisha wafundishe jinsi ya kutekeleza majukumu ya kazi unayowapa.
Mambo yatakuwa rahisi kuliko ukianza kuajiri ujuzi na uzoefu kisha kujaribu kufundisha tabia na mtazamo.

Pamoja na hayo yote, zoezi la kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wako linapaswa kuwa endelevu.
Kila wakati fundisha yote, yanayofundishika na yasiyofundishika.
Unachotaka ni mfumo wako sahihi ueleweke na wote.
Na wale wanaoshindwa kuelewa na kutekeleza, basi hawapaswi kuendelea kuwepo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe