2898; Muda upo.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayelalamika kwamba unachokosa ni muda ndiyo maana unashindwa kufanya yale unayopaswa kutafanya.
Hii ni sababu au kisingizio ambacho kila mtu huwa anakitumia.
Moja ya misingi yangu ni kwamba chochote kinachofanywa na wengi, hakiwezi kuwa sahihi kwako kupata matokeo bora.
Hivyo basi, inapokuja kwenye muda, malalamiko yako siyo sahihi.
Malalamiko kwamba hakuna muda siyo sahihi.
Muda upo, kinachotofautiana ni vipaumbele.
Wanaofanya makubwa huwa hawasubiri wapate muda. Badala yake huwa wanautenga muda na kuutumia kwa tija.
Kusema huna muda maana yake unasema huna vipaumbele.
Pia unaashiria kile unachokosa muda wa kukifanya siyo muhimu sana kwako.
Maana vitu vinapokuwa muhimu, muda wa kuvifanya huwa unapatikana.
Hata kama umetingwa kiasi gani, inapokuja kwenye mambo muhimu zaidi kwako, muda huwa unapatikana.
Hivyo futa kabisa msamiati wa huna muda. Anza kutumia msamiati wa muda upo kwa yale muhimu.
Ili uweze kuishi kwenye msamiati huo mpya, lazima uyaache mengi ya huko nyuma.
Huwezi kupata matokeo mapya kwa kuendelea kufanya yale ya zamani.
Anza na vipaumbele muhimu kwako na hivyo vitengee muda wa kufanya.
Kama unayofanya ndiyo muhimu zaidi kwako, yafanye mpaka kuyakamilisha.
Fanya jambo moja kwa wakati na weka umakini wako wote kwenye kile unachokuwa unafanya kwa wakati husika.
Na pale linapopatikana jambo jipya la kufanya, angalia kipaumbele cha jambo hilo kisha liweke sehemu sahihi kulingana na vipaumbele vya mengine uliyopanga kufanya.
Kama jambo unalopaswa kufanya siyo kipaumbele kwako, waeleze watu wazi kwamba hakipo kwenye vipaumbele vyako.
Hiyo inawasaidia kujua wategemee nini.
Muda upo na tena wa kutosha kabisa kama utaupangilia vyema kwa kutumia vipaumbele ulivyonavyo.
Pambana sana kushika hatamu ya muda wako, hapo ndipo penye nguvu ya kujenga au kubomoa maisha yako.
Usipoweka vipaumbele vyako kwa usahihi, utajikwamisha kwenye mengi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe