2901; Orodha na pesa.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayekuwa ‘bize’ kila siku lakini huoni hatua kubwa ambazo unazipiga.
Unakuwa ‘bize’ kweli kweli siku nzima, unakuwa huna muda kabisa.
Lakini ukiangalia matokeo unayozalisha, hayaonekani kabisa.
Kwa sehemu kubwa, wengi tumerithi mfumo wa kazi unaotumika kwenye ajira nyingi rasmi.
Kwenye ajira hizo, ufanyaji kazi wa mtu unapimwa kwa jinsi alivyo ‘bize’ muda mwingi.
Mfumo huo hauangalii mtu amezalisha matokeo ya aina gani.
Hivyo basi, kinchotokea ni watu kuhakikisha wanaonekana wako bize kweli kweli, lakini hakuna matokeo makubwa wanayozalisha.
Muda ni moja ya rasilimali muhimu na adimu. Unapaswa kuupangilia na kuutumia vizuri muda wako ili uweze kupiga hatua kubwa na zinazokupa mafanikio.
Mahali muhimu pa kuanzia kwenye muda ni kufanya kazi zako kwa orodha.
Kwa njia hii, unakuwa na orodha ya mambo muhimu kwako kutekeleza kisha unaifanyia kazi orodha hiyo.
Hapo unatekeleza yale yaliyo kwenye orodha yako kulingana na umuhimu wake na hurusu lolote nje ya orodha hiyo kukuvuruga.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuna uhusiano wa karibu kati ya kuwa na orodha ya mambo ya kufanyia kazi na kipato ambacho mtu anaingiza.
Kama hutekelezi majukumu yako kwa orodha, hutengenezi kipato kikubwa.
Hivyo basi, hatua ya kwanza na muhimu kwako kuongeza kipato chako mara moja ni kuanza kuweka orodha ya majukumu ya kutekeleza kulingana na umuhimu wake na kuifuata hiyo.
Ukishapangilia orodha yako, kuwa mkali nayo, usiende nje ya orodha hiyo. Labda kama kutatokea dharura ambayo ni kubwa.
Kuna mambo mengi ya kufanya kila siku na mengi yananyemelea sana muda wako.
Kama huna mfumo wa kuyapangilia mambo kulingana na umuhimu wake, utaishia kutingwa na mambo yasiyo muhimu sana na ambayo hayakupi matokeo makubwa.
Kwa uhaba mkubwa wa muda, unapaswa kuandaa orodha ya yale unayopaswa kutekeleza kulingana na umuhimu na matokeo unayotaka kuzalisha.
Unaweza kwenda mbali zaidi na kutenga muda wa kutekeleza kila jukumu lililopo kwenye orodha yako.
Hiyo inafanya siku yako nzima kuwa imepangiliwa na hivyo kupunguza sana upotevu wa muda.
Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda wao mwingi wa siku kwa kufikiria nini wafanye kati ya mengi yaliyo mbele yao.
Kama huridhishwi na matokeo unayopata sasa, anzia kwenye orodha yako ya mambo ya kukamilisha kila siku.
Kama huna kabisa, basi unajua shida inaanzia wapi.
Kama huwa unayo, angalia vigezo vyako vya umuhimu wa mambo.
Kama unataka kupata matokeo bora, kama unataka kuongeza kipato chako, pangilia orodha ya mambo muhimu ya kufanyia kazi kila siku na fuata orodha hiyo kwa nidhamu ya hali ya juu sana.
Majambazi wa muda wako ni wengi, silaha pekee kwako ni kuwa na orodha. Bila ya silaha hiyo, hutoboi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe