2905; Wanakudanganya.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayeshangazwa na jinsi ambavyo watu wanabadilika na kudanganya.

Unakuta unawaamini sana watu, lakini ghafla wanakuja kubadilika na kuwa wadanganyifu.

Ni vigumu sana kwa watu kubadilika ghafla.
Watu huwa wanang’ang’ana sana na tabia zao.

Hivyo kama kuna mtu unaona amebadilika, kwa sehemu kubwa anakuwa hajabadilika, bali ndivyo alivyokuwa tangu awali.

Kinachokuwa kimetokea ni awali ulidanganyika na kuwaamini. Kuna namna walikulaghai awali na wewe ukaamini. Halafu kuna kitu kikatokea ambacho kilikufanya uwe na wasiwasi kuhusu watu hao na hapo ndipo ukaanza kuona wanakudanganya.
Wewe unakuwa unaona wamebadilika, lakini kumbe ndivyo walivyokuwa muda wote.

Kuondokana na hilo na ili kuweza kuwa na utulivu na kufanya maamuzi sahihi, chukulia kila mtu kama anakufanganya.
Haimaanishi uwaambie ni waongo, bali unawachukulia hivyo ndani yako.

Kwa kuwachukulia watu hivyo, unachokuwa unaangalia ni ushahidi kama hawadanganyi.
Kwa njia hiyo utajionea vitu kwa uhalisia wake badala ya kuvurugwa.

Watu wanapotaka kukudanganya huwa kuna namna wanakuvuruga usiuone ukweli.
Usipokuwa makini, unanasa kwenye huo mvurugo wao na kushindwa kuona ukweli.

Lakini kwa kuanza na fikra kwamba wanakudanganya, utalazimika kutafuta ushahidi kwamba hawakudanganyi.
Na pale inapotokea ukagundua ni kweli wanakudanganya, hushtushwi wala kuona watu wamebadilika, bali unakuwa umethibitisha ulichokuwa unadhania muda wote.

Kama ambavyo wanasheria wanachukulia kila mtu ni mhalifu mpaka atakapothibitishwa siyo, ndivyo pia unavyopaswa kuchukulia kila mtu anakudanganya mpaka utakapothibitisha siyo.

Kumbuka hii ni njia ya kifikra na kimtazamo ya kukusaidia wewe usinase kwenye mitego ya watu kukudanganya.
Haimaanishi uwashutumu watu au kutokuwaamini kabisa.
Bali unajipa nafasi kwamba huenda wanadanganya.

Na kwa kanuni ya wastani, wengi watakuwa wanakudanganya kuliko wanaokuambia ukweli.
Maisha ni kama vita, siyo rahisi kumjua adui anayewinda kujinufaisha kupitia wewe.
Kadiri unavyokuwa na njia nyingi za kuwagundua wasio sahihi, ndivyo unavyoweza kuvuka mitego mingi unayokuwa umewekewa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe