2906; Kukosa subira kunakuponza.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayekata tamaa haraka pale unapokuwa huoni matokeo unayotaka licha ya kuweka juhudi kubwa.

Kuweka juhudi ni sehemu moja muhimu katika mafanikio. Na ndilo eneo pekee ambalo una udhibiti nalo.

Kuwa na subira ni eneo jingine muhimu sana kwenye safari ya mafanikio, eneo ambalo wengi ndiyo huwa wanashindwa.

Twende na mfano ili tuelewane vizuri.
Umeweka maji jikoni, kisha ukawasha kuni au mkaa.
Moto unawaka, lakini maji hayachemki.
Unadhani nini unapaswa kufanya ili hayo maji yachemke?

Iko wazi, unachohitaji ni kuendelea kuchochea moto na kusubiri maji yachemke.
Hakuna muujiza hapo.
Huhitaji elimu yoyote kubwa kujua hilo.
Chochea moto na kuwa na subira, hayo maji yatachemka tu.

Kadhalika, kwenye chochote unachofanya, kama juhudi unazoweka ni sahihi, unachohitaji ni subira tu, hakuna kingine chochote.
Wewe endelea kuweka juhudi bila kuchoka na kwa wakati sahihi matokeo unayoyataka yatakuja.

Hebu fikiria, umewasha moto na kuweka maji, ukaona hayachemki, ukayaepua, unakuwa umerudi nyuma zaidi. Kwani hata lile joto ambalo lilikuwa limeanza kujijenga, litapotea, ukianza kuyachemsha tena unaanzia chini zaidi.

Usiache kuweka juhudi kwa sababu huyaoni matokeo, wewe endelea na juhudi huku ukiboresha zaidi.
Yaani juhudi ziendelee, usipoe hata kidogo, utajirudisha nyuma zaidi.

Moja ya vitu ambavyo vimeharibu sana akili zetu kwenye zama hizi ni simu janja na mitandao ya kijamii.
Teknolojia hizi zimerahisisha sana raha, yaani unaipata raha kwa haraka mno.
Hilo limefanya tuone kila kitu kwenye maisha kinapaswa kuja haraka kwa namna hiyo. Kitu kikichelewa kidogo tu tunaona hakiji kabisa.
Tuliepuke hili kwa kuelewa kanuni za asili, vitu vinavyodumu vinachukua muda kujengeka.

Mpapai unaota na kutoa matunda haraka, lakini maisha yake ni mafupi.
Mbuyu unachelewa sana kuota na kutoa matunda, lakini maisha yake ni marefu.
Jiulize wewe unaotesha nini, mpapai au mbuyu?

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe