2908; Mabadiliko.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayeona mabadiliko ni magumu kuliko mazoea uliuokuwa nayo awali.
Hilo ni kweli,
Kwa mtazamo wa haraka haraka, mabadiliko huwa yanaonekana ni magumu na mabaya.
Huwa ni vigumu sana kuachana na kile ambacho mtu umeshakizoea na kwenda kwenye kitu kipya ambacho hakijazoeleka.
Ulichokizoea, hata kama hakikupi matokeo makubwa, unakuwa na uhakika nacho.
Lakini kipya, hata kama kina ahadi ya kuleta matokeo makubwa, kina hatari na huna uhakika.
Ili uweze kuyapokea mabadiliko, lazima kwanza uondoe dhana ya uhakika.
Anza kwa kujua kwamba hakuna kitu chochote chenye uhakika wa asilimia 100.
Hata kile ulichozoea, bado hakina uhakika wa asilimia 100.
Chochote kinaweza kutokea na kuvuruga mazoea na uhakika uliokuwepo.
Ukishajua hakuna chenye uhakika, unakuwa tayari kubadilika na kujaribu vitu vipya.
Imekuwa inasemwa, ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile halafu kutegemea matokeo ya tofauti.
Na hilo ndiyo chanzo cha wengi kushindwa kufanikiwa kwenye maisha yao.
Watu wanapenda kupata matokeo ya tofauti, lakini hawapo tayari kubadilika.
Huo ndiyo ujinga unaoelezwa hapo.
Kama unataka kupiga hatua, jiambie wazi; NAACHA UJINGA. SITAENDELEA NA MAZOEA HALAFU NITEGEMEE MAFANIKIO.
Anza vita na mazoea.
Hata bila ya sababu yoyote ya msingi, acha mazoea yoyote uliyonayo.
Weka utofauti na upekee kwenye kila unachofanya.
Ndiyo, unatembea kwa miguu kama watu wengine, lakini hebu tembea ukiwa wima, ukingalia mbele na kwa kujiamini.
Tembea kama mtu anayejua wapi anaenda na usiwe kama mzururaji tu.
Ni kweli utaongea kwa mdomo kama ambavyo umekuwa unafanya, lakini hebu ongea kwa shauku kubwa mpaka anayekusikiliza aseme huyu mtu ameongea kitu cha maana kwangu.
Ongea kama mtu unayejua unachoongea na usiwe kama mropokaji tu.
Badilika.
Kwenye kila unachofanya.
Hutapata matokeo ya tofauti kwa kuendelea na hayo mazoea.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe