2910; Wakati sahihi wa kutafuta kitu.
Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye umekuwa unakutana na changamoto kubwa kwenye mambo unayokuwa unayataka.
Umekuwa unasubiri mpaka pale unapokihitaji kitu kwa haraka ndiyo unahangaika kukitafuta.
Kwa haraka unayokuwa nayo, unajikuta ukishindwa kuzingatia mambo muhimu na hilo linapelekea ufanye makosa.
Wakati sahihi wa kutafuta kitu ni pale unapokuwa huna uhitaji nacho wa haraka.
Hilo linakupa uwanja mpana wa muda na kuweza kuzingatia yote yaliyo muhimu.
Unakuwa na muda wa kufanya uchunguzi wa kutosha kabla hujafanya maanuzi.
Asili huwa inafanya kazi kwa namna ya ajabu. Pale unapokuwa na uhitaji mkubwa wa kitu, inakuwa vigumu sana kwako kukipata. Lakini pale unapokuwa huna uhitaji mkubwa wa kitu, kinakuja kwako kwa urahisi zaidi.
Tuchukue mfano wa kuajiri kwenye biashara. Unapotafuta mfanyakazi pale unapokuwa na uhitaji mkubwa inakuwa vigumu sana kupata mfanyakazi bora. Kwani unajikuta ukiharakisha na kuvuka baadhi ya mambo muhimu ili tu upate mfanyakazi unayemtaka.
Kinachotokea ni yanakuwa majanga, mfanyakazi unayempata anakuwa siyo sahihi.
Lakini unapotafuta mfanyakazi wakati ambao huna uhitaji wa kuajiri, unajipa muda wa kutosha wa kufanya uchunguzi na kumpata aliye sahihi zaidi.
Chochote unachojua utakuja kukihitaji huko baadaye, anza mapema kukifanyia kazi. Kadiri unavyokuwa na muda mwingi wa kufanyia kitu kazi, ndivyo unavyopata fursa ya kukifanya kwa ubora wa hali ya juu.
Mara zote kuwa na mipango mizuri inayokupa maandalizi ya kutosha kwenye chochote unachokuwa unataka.
Na muhimu zaidi, jizuie kuharakisha kwenye maamuzi yaliyo muhimu, unatengeneza matatizo yanayokusumbua sana.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe