2911; Misingi.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayeona mambo ni magumu na mafanikio hayawezi kufikiwa.

Jambo la kwanza ninalotaka kukuhakikishia ni kwamba mara zote mafanikio huwa yapo.
Yaani hata mambo yawe magumu kiasi gani, bado mafanikio yapo.
Hata hali ya uchumi iwe ngumu kiasi gani, mazingira yawe magumu kiasi gani, mafanikio yameendelea kuwepo.

Dunia imepitia mengi magumu, maanguko ya kiuchumi, vita za dunia na milipuko mikubwa ya magonjwa, lakini katika nyakati zote hizo, mafanikio pia yamekuwepo.
Pamekuwa na watu waliofanikiwa sana katika nyakati hizo ngumu ambazo ziliwakatisha tamaa wengi.

Jambo la pili ni misingi ya mafanikio haijawahi kubadilika. Misingi mikuu ya mafanikio imekuwa ile ile tangu enzi na enzi.
Licha ya zama kubadilika na teknolojia kurahisisha mambo mengi, bado misingi ya mafanikio ni ile ile.
Mikakati na mbinu vinabadilika, lakini misingi ni ile ile.

Chukua mfano wa kuandika, kuandika ni kule kule.
Kuna kipindi watu walikuwa wanaandika kwenye mawe, ikaja kuandika kwenye karatasi na sasa kuandika kwenye vifaa vya kielektroniki. Mbinu zimebadilika, lakini msingi ni ule ule.

Watu wengi wamepotoshwa sana kimafanikio kwa kupuuza haya mawili uliyojifunza hapa.
Wengi sana wanakatishwa tamaa na nyakati ngumu na kuona mafanikio hayawezekani tena.
Wewe usikubali hili, jua mafanikio yapo nyakati zote na wewe utayapata kwa uhakika.

Halafu wengi zaidi wameyakosa mafanikio kwa kupuuza misingi kwa kuamini kwamba mambo yamebadilika. Wanaachana na misingi na kukimbilia mbinu mpya, mwishowe wanaangukia pabaya.
Kwa mfano moja ya misingi muhimu ya mafanikio kifedha ni kutoa thamani. Kwamba unalipwa kulingana na thamani unayotoa kwa wengine.
Miaka ya karibuni zimegundulika sarafu za kidijitali ambazo zimekuwa hazina thamani yoyote kimatumizi kwa watu, lakini kwa tamaa, bei zake zinakuwa kubwa.
Wengi wakaona ni njia ya kupata utajiri wa haraka bila kufanya kazi, wakazinunua kwa wingi, mwishowe zikakosa thamani na wakapoteza kila siku.

Asikudanganye mtu, hakuna misingi mipya. Misingi ni ile ile. Kama akija mtu kwako na kukuambia amegundua misingi mipya, jua wazi anataka kukulaghai.

Kuna sababu kwa nini vitabu vya dini na falsafa vimeendelea kukubalika japo vimeandikwa miaka mingi sana iliyopitwa. Kwa sababu vimejengwa kwenye misingi fulani isiyopitwa na wakati.
Japo wakati vitabu hivyo vinaandikwa hakukuwa na teknolojia zilizopo sasa, bado maarifa yake yamekuwa na manufaa kwenye teknolojia tulizonazo.
Kwa sababu yamejengwa kwenye misingi sahihi.

Kama kuna kitu kimoja cha kufanya ambacho kitakuhakikishia maisha ya mafanikio ni kuiishi na kuisimamia misingi nyakati zote.
Hasa pale mambo yanapokuwa magumu, ndiyo wakati muhimu zaidi kwako kuisimamia misingi.
Wengi huyumba kwenye misingi pale nyakati zinapokuwa ngumu, wewe usiwe hivyo.

Jua mafanikio yapo nyakati zote na misingi ya mafanikio haibadiliki.
Ifuate misingi ya mafanikio kama saa mbovu na lazima utafanikiwa, hata mambo yawe magumu kiasi gani.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe