2913; Muhimu zaidi.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayesema unatingwa na mambo mengi kwenye biashara.

Napenda kukuuliza, katika mengi yanayokutinga, mangapi ndiyo muhimu kabisa?

Ni mambo yapi machache ambayo ukikusanya nguvu zako hapo unapata matokeo makubwa?

Na muhimu zaidi, jambo lipi moja ambalo ukilipa kipaumbele cha kwanza, linaweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye biashara yako?

Hayo ni maswali ambayo unapaswa kuwa na majibu yake kwa uhakika kama kweli umedhamiria kufanya makubwa.

Na kama huna majibu ya maswali hayo, hapa nakusaidia swali moja muhimu la kipaumbe cha kwanza.

Kuna mambo mengi ya kufanya kwenye biashara, ambayo mengi yatakuhitaji. Lakini mambo hayo hayalingani.

Jambo moja ambalo ukilipa kipaumbele na kuliwekea juhudi kubwa linaweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye biashara yako na kwako binafsi ni mauzo.

Mauzo ndiyo moyo wa biashara.
Mauzo ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara.
Kwa umuhimu huo mkubwa wa mauzo, ungetegemea kila mfanyabiashara ayafanye mauzo kuwa kipaumbele cha kwanza kabisa kwake.

Lakini kitakachokushangaza ni jinsi ambavyo mauzo yamekuwa hayapewi kipaumbele kikubwa na wafanyabiashara walio wengi.

Mafanikio ya biashara yanaanzia kwenye mauzo.
Na utajiri mkubwa unatengenezwa kupitia mauzo.

Sababu kwa nini wafanyabiashara wengi bado hawapati mafanikio makubwa wanayotaka ipo wazi, wanahangaika na mengi sana yasiyokuwa na tija.
Wanasahau kitu kimoja muhimu sana ambacho ni mauzo.

Wanatawanya nguvu zao kwenye majukumu mengi, ambayo hayana nguvu ya kuleta matokeo makubwa.

Leo ninachokuambia ni kimoja, sehemu pekee ya kupeleka muda wako, nguvu, akili, ubunifu, kazi na rasilimali zako zote ni kwenye mauzo.

Hicho ndiyo kipaumbele cha kwanza kabisa ambacho ukikifanyia kazi lazima upate matokeo makubwa na ya tofauti.

Kama biashara yako ina changamoto zozote zile, sehemu pekee ya kuanza kufanyia kazi ni mauzo.
Mauzo yana nguvu ya kutatua changamoto nyingi sana za kibiashara.

Na kama kuna changamoto ambayo biashara inapitia na haiwezi kutatuliwa na mauzo, changamoto hiyo haiwezi kutatuliwa na kingine chochote.

Usitawanye hovyo nguvu zako kwenye biashara, badala yake zikusanye eneo moja muhimu zaidi ambalo ni mauzo.

Gatua majukumu yako yote ya kibiashara na ubaki na jukumu moja tu, la kuuza.

Naamini unajua ninaposema mauzo au uuze simaanishi kupokea fedha za wateja na kuwapa kile wanachotaka.
Kama hivyo ndivyo unavyodhani, tayari umeshapotea.

Wewe wajibu wako ni kuiuza biashara nzima, kuwauzia wateja moja kwa moja ni majukumu unayoweza kuwapangia wengine na wakayafanya vizuri.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe