2919; Watatenganishwa na fedha zao.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayewaonea wateja huruma na fedha zao.
Wateja wanakuambia hawana fedha au wamebaki na fedha kidogo na wewe unaona hupaswi kuwamalizia fedha zao kwa kuwauzia unachouza.
Kama utayaendea mauzo na wateja kwa mtazamo huo, kamwe hutouza. Mauzo yatakuwa magumu sana kwako kwa sababu kuu mbili.
Moja ni wateja huwa wanadanganya, hivyo kwa sehemu kubwa wanayokuambia siyo kweli.
Mbili ni wateja watatenganishwa na fedha zao kwa namna yoyote ile. Hata kama hutawauzia wewe, bado kuna watu watawashawishi na kuwauzia na hivyo kuwatenganisha na fedha zao.
Hivyo wewe kudhani unawaonea wateja huruma kwa kutokuwauzia huwasaidii, bali unazidi kuwaumiza.
Unawaumiza kwa sababu unaacha kuwauzia kitu ambacho ni muhimu na kina manufaa kwao. Halafu wanaenda kuuziwa kitu cha hovyo na kuwa wamepoteza fedha zao.
Kama kweli unaamini kile unachouza na unajua kina manufaa kwa mteja wako, basi ni wajibu wako wa kimaadili kuwauzia unachouza, bila kujali hali yao kifedha.
Ni wajibu wako wewe kuwashawishi waione thamani kubwa uliyonayo na jinsi ina manufaa kwao ili wafanye maamuzi sahihi ya kukinunua.
Usiishie tu kusema shauri yake kama hataki, ni wajibu wako kumpa mteja mapendekezo ya kile kilicho bora kwake na kuhakikisha anakipata kwa manufaa yake.
Sehemu kubwa ya kazi ya mauzo ni kuwasaidia wateja kufanya maamuzi kwenye mambo ambayo ni muhimu na yenye manufaa kwao.
Wewe kama mtu wa mauzo utakuwa unajua vitu vingi kuliko mteja kwenye kile unachouza. Unapaswa kutumia ujuzi huo kuwashawishi wateja wanufaike na kile unachouza.
Kwa kuwa wateja watatenganishwa na fedha zao, iwe watanunua kwako au la, ni wajibu wako kuhakikisha wamenunua kwako kwa sababu ndiyo utakuwa uwekezaji bora wa fedha zao ambao hawataujutia.
Kama kweli huamini kile unachouza na kuona wateja wanapaswa kuwa nacho kwa sababu ndiyo kipaumbele sahihi kwao, basi hupaswi hata kukiuza kabisa.
Itakuwa vigumu sana kwako kuuza kitu ambacho huna imani nacho na huoni kikiwa ndiyo muhimu zaidi kwa wateja.
Mauzo ni mabadilishano ya imani na shauku. Lazima uwe na imani na shauku kubwa wewe muuzaji ndiyo uweze kuviambukiza kwa mteja na asukumwe kununua.
Kwa kuzingatia haya tuliyojifunza hapa, kila mtu wa mauzo ana majukumu makubwa matatu;
Moja ni kujua thamani kubwa iliyopo kwenye kile ambacho anauza. Kuelewa kwa kina, kuamini na kuwa na shauku kubwa.
Mbili ni kuchagua watu sahihi wa kuwauzia, ambao wana maumivu yanayotatuliwa na thamani hiyo. Hakuna kitu chochote kinachoweza kumfaa kila mtu. Hivyo kabla ya kuuza, lazima uchagua wale ambao watanufaika sana.
Tatu ni kuwaonyesha unaowalenga thamani iliyopo na jinsi ilivyo na manufaa kwao na hawapaswi kuikosa. Hapa unapaswa kuwaonyesha wateja hao wanafanya makosa makubwa kama hawanunui kile unachowapendekezea.
Kwa kuzingatia haya matatu, mauzo yatakuwa rahisi na makubwa kwako. Hayatakuwa rahisi kwamba hayahitaji kazi, bali yatakuwa rahisi kutokana na kazi kubwa unayokuwa umeifanya.
Kama unayo thamani yenye manufaa kwa mteja, kushindwa kumuuzia ni dhambi kubwa sana kwako. Ni wajibu wako kuhakikisha mteja anaipata thamani uliyonayo, kwani usipomuuzia wewe, ataenda kuuziwa vitu visivyo sahihi na watu wengine.
Kumuuzia mteja, humsaidii tu kwa kumpa thamani uliyonayo, bali pia unamsaidia kwa kumwepushia upotevu wa fedha zake kwenye vitu visivyokuwa muhimu kwake.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe