2922; Mambo yanapokuwa magumu.
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye hii safari ya mafanikio, mara nyingi utakutana na mambo magumu na changamoto.
Hata pale unapokamilisha mipango unayokuwa umejiwekea, kufurahia huwa ni kwa muda mfupi. Baada ya hapo unapaswa kurudi kwenye kupambania malengo na mipango mikubwa zaidi ya uliyofikia.
Kitu ambacho kifakupeleka kwenye magumu na changamoto mbalimbali.
Ambacho nimekuwa naona kwa wengi ni wanakata tamaa pale wanapokutana na magumu na changamoto. Wengi wanaacha kukaa kwenye mchakato tulio nao.
Na hilo ndiyo linafanya mambo yao kuwa magumu zaidi.
Rafiki, mambo yanapokuwa magumu na unapokutana na changamoto mbalimbali, huo ndiyo wakati wa kukaa zaidi kwenye mchakato.
Hiyo ni kwa sababu kukaa kwenye mchakato kunakupa utulivu na mpango wa kukabiliana na magumu au changamoto unazokuwa umekutana nazo.
Usimkimbie kocha wako pale mambo yanapokuwa magumu. Badala yake huo ndiyo wakati wa kujenga naye ukaribu ili kwa pamoja muweze kuyavuka magumu unayokuwa unayapitia.
Kocha siyo mtu wa kumpa habari njema pekee, bali ni mtu wa kumshirikisha habari mbaya nyingi unazokuwa unakabiliana nazo.
Kuuacha mchakato wakati unapokuwa kwenye matatizo au changamoto ni kujisalimisha kwenye matatizo hayo na kuyapa ushindi juu yako.
Kama kuna tatizo au changamoto unayokutana nayo na ukaona haiwezi kutatuliwa kwa kukaa kwenye mchakato, basi pia hutaweza kuitatua ukiwa nje ya mchakato.
Wakati mwingine unaweza kujishawishi wacha nikae nje ya mchakato kidogo nitatue yanayonikabili halafu nitarudi.
Ukihadaika tu na hayo mawazo ndiyo unakuwa umepoteza moja kwa moja.
Ukishauacha mchakato sahihi, kushindwa ni uhakika na kurudi tena kwenye mchakato huo kunakuwa kugumu sana.
Kama kweli umedhamiria kuyapata mafanikio makubwa unayoyataka, jua magumu na changamoto ni sehemu ya safari hiyo na jipe kiapo cha kuendelea kukaa kwenye mchakato hata mambo yawe magumu kiasi gani.
Unapaswa kukaa kwenye mchakato kwa msimamo kama saa mbovu ya mshale. Haijalishi unapitia magumu na changamoto kiasi gani, wewe unaendelea kukaa kwenye mchakato wako kamili bila kuyumba.
Unaendelea kumtumia vyema kocha wako ili uweze kuyavuka magumu na changamoto mbalimbali zinazokukabili.
Kwa kuwa safari ya mafanikio ni ya changamoto baada ya changamoto, kuzalisha tatizo jipya pale unapovuka tatizo la zamani, suluhu yako ipo kwenge kukaa kwenye mchakato kwa msimamo bila kuyumba.
Ni kukaa kwenye mchakato ndipo kunakuwezesha kukabiliana na lolote linalokutana nalo kwenye safari ya mafanikio.
Ninakuhitaji zaidi pale mambo yako yanapokuwa magumu kuliko hata mambo yako yanapokuwa marahisi.
Maana wakati wa mambo rahisi kila mtu anaweza kuonekana anakwenda vizuri.
Lakini pale mambo yanapokuwa magumu na yenye changamoto ndiyo uhalisia unapoonekana wazi.
Wewe kaa kwenye mchakato mara zote bila kuyumbishwa, hakuna kitakachoweza kukushinda.
Kwani hata ukishindwa kukitatua kwa njia ulizonazo, muda huwa ni tatibu mzuri wa chochote kile. Kwa kukipa kitu muda huku unaendelea kukaa kwenye mchakato, unakipa nafasi ya kujitatua chenyewe.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe