2930; Kokotoa thamani ya muda wako.

Rafiki yangu mpendwa,
Kupitia kurasa hizi nilikushirikisha dhana ya kuwa na thamani ya muda wako ili uweze kuutumia vyema.
Dhana hiyo ilihusisha kuupa muda thamani ya kifedha ili kutokuupoteza kwa mambo yasiyo na tija.

Wengi hawakuelewa jinsi ya kuweza kukokotoa thamani ya muda wao.
Leo unakwenda kujifunza jinsi ya kufanya hivyo.

Ukokotoaji huu wa thamani ya muda unahusisha hesabu, kitu ambacho kinaweza kisiwe pendwa kwa wengi.
Hivyo kama hizo hesabu zitakuchanganya, wewe chukulia thamani ya saa moja kuwa Tsh laki moja.
Hiyo ni namba nzuri ya kuanzia ambayo itakusukuma sana kwa yale unayofanya.

Sasa kwa wale ambao wangependa kujua hesabu za kukokotoa thamani ya muda kwa uhakika.

Kwanza unaanza na kipato ambacho unapanga kuingiza kwa mwaka, kisha unagawa kwa mwezi kisha wiki na hatimaye siku.
Kwa upande wetu litakuwa ni lengo la mauzo.

Ukishajua kiwango hicho kwa siku, kigawe kwa masaa ya kazi kwa siku.
Japokuwa tunapanga muda wa kazi kuwa masaa 16 kwa siku, siyo yote utaweza kuyatumia kwa mambo yanayozalisha tu. Kuna mambo mengine utalazimika kufanya ambayo hayawezi kuchangia kipato moja kwa moja.

Hivyo katika masaa 16 ya kazi kwa siku, chukulia 10 ambayo ndiyo unayaweka kwenye majukumu yanayochangia kwenye fedha moja kwa moja.
Hivyo lengo lako la kipato kwa siku gawa kwa masaa 10 na hapo utapata thamani ya saa yako moja.

Kwa mfano kama kwa kugawa lengo lako umepata milioni 1 kwa siku kama ndiyo lengo la mauzo, basi thamani ya saa yako moja ni milioni 1 gawa kwa 10 ambapo inakuwa ni lako moja.

Sasa basi, japo umegawa thamani ya muda kwenye masaa 10 ya siku, bado hiyo ndiyo utakayoitumia kwa masaa yote 16 ya siku.
Hivyo kwa kila unachofanya kwenye masaa hayo 16 jiulize kinamchango gani katika kuingiza tsh laki 1?

Kama kitu hakina thamani hiyo basi hukifanyi. Kama unachotaka kufanya hakiingizi fedha au kukuandaa kuingiza kiasi hicho cha fedha, unapaswa kuacha kukifanya.

Pia thamani ya muda wako itakusaidia kujua majukumu yapi uyafanye na yapi uwape wengine wafanye.
Kwa sasa, kuna majukumu unahangaika kuyafanya, ambayo ni muhimu yafanyike, lakini kuna wengine wangeweza kuyafanya kwa gharama ndogo zaidi.

Chukua mfano wa kufyeka nyasi nyumbani kwako. Ni jukumu muhimu kufanyika. Ukilifanya mwenyewe litakuchukua siyo chini ya saa moja. Ukiweka kibarua wa kulifanya, atakutoza elfu 10.
Sasa hapa ndipo wengi wanapopoteza, anaona elfu 10 ni kubwa, anaweza kufanya kazi hiyo mwenyewe.
Hivyo anaacha kumpa mtu elfu 10 afanye hiyo kazi na kukazana kuifanya mwenyewe.
Anajiona ni shujaa aliyeokoa fedha, ila haoni fedha nyingi alizopoteza kama angemwajiri kibarua afanye kazi hiyo, kisha yeye akatumia muda huo kukamilisha mauzo zaidi.

Jipime kila saa mwa majukumu unayofanya na jiuljze yanachangiaje kwako kufanya mauzo yanayoendana na thamani ya muda wako.
Inaweza isiwe kuuza moja kwa moja, lakini ikawa ni kufanya maandalizi ya mauzo ambayo baadaye yatawezesha kukamilisha mauzo hayo.

Kokotoa thamani ya muda wako na hakikisha chochote unachofanya kinaendana na thamani hiyo ya muda.

Ili uone uchungu wa jinsi unapoteza muda wako mwingi kwa mambo yasiyokuwa na tija, nimekupa utaratibu mwingine.
Utaratibu huo ni kuorodhesha saa kwa saa jinsi unavyotumia muda wako wa masaa 16 kwa siku.
Orodhesha masaa hayo yote, kuanzia saa kumi alfajiri mpaka saa mbili usiku.
Pangilia kila utakachofanya kwenye masaa hayo kulingana na thamanj yake katika kuchangia lengo la mapato.

Rafiki, usijiendee tu kwa mazoea, badala yake pima kila kitu. Namba huwa hazidanganyi, hivyo simama kwenye namba mara zote.

Kama haya mahesabu yamekuvuruga, achana nayo, wewe anza na thamani ya muda wako kuwa ths laki moja kwa saa.
Hivyo chochote unachofanya kiwe kinaingiza laki moja au kuandaa mazingira ya kuweza kutekeleza hilo baadaye.
Kwa mfano kwenye mauzo, unaweza kwa sasa usiwe kufanya mauzo ya laki moja kila saa.
Lakini kama utatumia muda huo vizuri kwenye masoko na mauzo, utaweza kutengeneza wateja tafajiwa wengi zaidi na kuwashawishi kununua.

Anza na namba, kisha utakua kuanzia hapo.
Kama huna namba unazojipima nazo, hakuna namna unaweza kukua.
Na namba ya msingi kabisa ni thamani ya muda wako.
Hiyo ndiyo itaweza kukufungua macho na kukuonyesha wapi unapoteza muda na fedha pia.

Muda ni rasilimali adimu sana, yenye thamani kubwa kuliko hata fedha. Ukipoteza fedha unaweza kuzipata tena, ila ukipoteza muda ndiyo umeupoteza moja kwa moja.
Hivyo badala ya kutumia muda kuokoa fedha, mara zote tumia fedha kuokoa muda.
Maana yake usifanye lolote ambalo thamani yake ni chini ya thamani ya muda wako, hata kama muda unao na fedha huna.
Badala ya kuuchezea muda huo, upeleke kwenye mambo yatakayoweza kukupa thamani kubwa zaidi.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe