2938; Mfalme ni mmoja tu kwenye biashara.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila himaya huwa inakuwa na mfalme mmoja tu.
Na neno la mfalme huwa ndiyo sheria, hufuatwa na kila mmoja.

Kwenye biashara pia kuna mfalme mmoja anayepaswa kuheshimiwa na wote.
Mfalme huyo ni MAUZO.

Kwa kuwa mauzo ndiyo kitu pekee kinachoingiza fedha kwenye biashara, kinapaswa kuheshimiwa sana.

Hivyo kipaumbele cha kwanza kwenye kila biashara kinapaswa kuwa ni mauzo.
Mauzo yanapaswa kuheshimiwa na kuwekewa juhudi kubwa.

Kama mmiliki na kiongozi wa biashara, mauzo ndiyo wajibu wa kwanza kwako.
Unapaswa kuhakikisha hakuna kikwazo chochote kinachokwamisha mauzo kwenye biashara yako.

Unapaswa kuwa mstari wa mbele kwenye mipango na mikakati yote ya mauzo.
Unapaswa kujua kila kinachoendelea kwenye mauzo ili kuhakikisha mauzo yanakuwa juu mara zote.

Chochote kinachopaswa kufanyika ili mauzo yaongezeke, unahakikisha kinafanyika kweli.
Kama inabidi kuongeza fedha, kuboresha bidhaa/huduma, kubadili watu, kuwapa mafunzo au chochote kingine, unahakikisha yanafanyika ili mauzo yaweze kuwa vizuri.

Mauzo ndiye mfalme kwenye biashara na wewe ndiye muuzaji namba moja.
Kama biashara haiuzi vizuri, lawama zote unazibeba wewe.
Kwa sababu unakuwa hujaweka umakini na juhudi za kutosha kwenye eneo hilo muhimu na namba moja kwenye biashara.

Hata kama umeajiri watu wa mauzo na ukaweka mtu wa kusimamia kitengo hicho, bado wewe mmiliki na kiongozi wa biashara unawajibika moja kwa moja kwenye mauzo.
Unapaswa kujua kila kinachoendelea kwenye mauzo.
Unapaswa kuzijua namba zote mnazojipima nazo kwenye mauzo na mwenendo wenu.
Na unapaswa kuanzisha na kusimamia mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mauzo yanakuwa makubwa zaidi.

Kwenye biashara, mauzo ndiye mfalme kwa sababu yanaleta fedha, hivyo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwenye biashara.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe